NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WARAIBU wa mihadarati wanaohitaji usaidizi wa kuacha kutumia dawa za kulevya kupitia dawa ya ‘Methadone’ hadi kufikia Juni mwaka huu wamefikia idadi ya 3,840 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hayo yamebainishwa leo Julai 17,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Janabi amesema idadi hiyo imeongezeka na kufanya Muhimbili kuwa kituo chenye idadi kubwa ya watu wanaofika ambao wameathirika na dawa za kulevya na wanahitaji dawa ya Methadone.
“Kwa siku tu jumla ya waatihirika wanaofika hospitalini Muhimbili ni 900 na wanakuja ili wapatiwe huduma ya methadone, ili bahati mbaya wanaokuja kupata tiba hospitalini hapo wanatushang’aza na hatujui tunawatibu kwa namna gani maana hatuelewi mchanganyiko wa dawa waliotumia,” amesema Janabi
“Nasema hivyo kwa sababu mtu akipata athari ya dawa za kulevya najua nimpatie dawa gani kumtibu sasa kama kutakuwa kuna mtu anatengeneza dawa huko za kulevya kwa kuchanganya dawa tiba mbalimbali hii inatuwia vigumu kumtibu mgonjwa,” amesema
Amesema dawa za kulevya zinasababisha athari katika mfumo wa umeme wa binadamu katika moyo, kufeli kwa figo na wakati mwingine waathirika kupata saratani ya homa ya ini na kuharibika kwa akili.