NA TERESIA MHAGAMA, BUKOMBE
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, DkDoto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini kutoka madhehebu
mbalimbali wilayani Bukombe pamoja na Wazee wa wilaya hiyo, katika
mkutano uliolenga kubadilishana mawazo na kumshukuru Mungu kwa mwaka
2023.
Mkutano huo umefanyika Desemba 31, 2023, Ushirombo wilayani
Bukombe mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama
cha Mapinduzi na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe,
Sakina Mohamed ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya
Bukombe.
“Mimi pamoja na wenzangu serikalini tunawashukuru sana wazee na
viongozi wa dini wa Bukombe kwa ushirikiano mkubwa mnaotoa kwetu, leo
nimeona tupate nafasi ya kumshukuru Mungu pamoja na ninyi na
kubadilisha mawazo kwani hakuna kiongozi anayeweza kufanya jambo
lolote bila kushirikishana na wenzake, ninyi mmeona mengi kuliko mimi,
mnafahamu mengi, mnajua mengi, uelewa wenu ni mkubwa na pia mnakaa na
jamii muda wote hivyo mnafahamu wapi turekebishe ili tutengeneze
Bukombe bora zaidi.” alisema Dk.Biteko
Ili kuwa na jamii iliyo bora, Dk. Biteko amewaasa viongozi hao wa
dini na wazee kuendelea kukemea matendo mabaya pale wanapoyaona, tena
bila kuyaonea aibu kwani ni watu wanaoheshimika katika jamii na
ujumbe kutoka kwao unawafikia watu wengi.
Pamoja na kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
wilayani Bukombe ikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Hospitali, usambazaji
umeme na barabara, Dk. Biteko amesema kuwa, changamoto zozote ambazo
bado zipo wilayani humo zitatatuliwa ili Bukombe iweze kuwa bora
zaidi.
Katika mwaka 2024, Dk. Biteko ametoa ujumbe wa watu wa makundi yote
kupendana na kusameheana na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha
inatoa huduma bora kwa wananchi ili watoto wasome kwenye shule nzuri,
wananchi watumie barabara nzuri, wahudumiwe katika zahanati, kituo cha
afya na hospitali nzuri, wapatiwe huduma ya umeme na maji hali
itakayofanya pia watu kupenda maeneo walikotoka.
Kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, Wazee wa Bukombe walipata
fursa ya kutoa maoni yao kuhusu maeneo ambayo wanaona kuwa yanahitaji
uboreshaji na pia walimpongeza Dk Biteko kwa kuwapa nafasi za
kuwasikiliza na kutoa ufafanuzi wa hatua mbalimbali ambazo Serikali
inachukua ili kuboresha huduma kwa wananchi wilayani Bukombe.