NA TERESIA MHAGAMA, BUKOMBE
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema
kuwa, Serikali inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Sekta
za kidini katika kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi mjini na
vijijini.
Dk Biteko amesema hayo leo Januari 2, 2024 wakati alipotembelea
Hospitali ya San Pio iliyopo wilayani Bukombe mkoani Geita akiwa
ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella na viongozi wa
Chama cha Mapinduzi. Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 2000 kwa
mwaka.
Kwa kutambua mchango huo wa Sekta za Kidini, Dk. Biteko amesema kuwa,
Serikali ipo tayari muda wote kushirikiana nao ili kuendeleza yale
wanayokusudia kuyafanya katika jamii.
Dk. Biteko amepongeza uongozi na wafanyakazi wa Hospitali hiyo chini
ya Mkurugenzi, Sista Teresa Goska, kwa kutoa huduma bora za kiafya kwa
wananchi na pia uamuzi wao wa kuanza kutoa huduma katika Sekta ya
Elimu ambapo wameanza na darasa la awali.
Akiwa katika Hospitali hiyo ya San Pio, Dk. Biteko aliwafariji
wagonjwa mbalimbali waliolazwa na wanaosubiri huduma pamoja na kukagua
majengo na miundombinu ya kutolea huduma hospitalini hapo.
Uongozi wa Hospitali hiyo umemshukuru Dk Biteko kwa kutembelea
hospitali hiyo ikionesha kuwa, anatambua na kuthamini huduma
inayotolewa kwenye hospitali ya San Pio ambayo ipo chini ya Jimbo
Katoliki la Kahama.