NA MWANDISHI WETU, MBEYA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia kijana aitwaye Humphrey Kihali F [25] Mkazi wa Ilemi jijini Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya baba yake mzazi aitwaye Francis Kihali [50] .
Awali Septemba 10, 2023 majira ya saa 10:45 jioni huko eneo la Ilemi mtuhumiwa alimvizia baba yake mzazi Kihali akiwa chumbani kwake na kisha kumpiga kwa kutumia ubao ambapo alikimbizwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na kufariki dunia leo Septemba 11, 2023 majira ya saa 1:30 asubuhi.
Pamoja na uchunguzi wa awali kubainisha kuwa mtuhumiwa ana tatizo la akili, uchunguzi unakamilishwa ili hatua zingine za kisheria zifuate.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wazazi na walezi ambao wana changamoto ya watoto wenye matatizo ya Afya ya Akili kuchukua tahadhari kwa kuweka uangalizi madhubuti na kufuata maelekezo ya utumiaji wa dawa wanazopewa ili kuzuia madhara makubwa kama haya yasitokee.