NA MWANDISHI WETU, TANGA
MKUU wa Wilaya ya Tanga mkoani Tanga Hashim Mgandilwa amewaomba viongozi wa dini kuzidisha juhudi za kukemea matendo vyenye viashiria vya ukatili wa kijinsi ili idadi ya matukio ya ukatili wa watoto na wanawake yaweze kupungua
Akifungua Kikao cha Viongozi wa Dini mbali mbali Jijini Tanga, DC Mgandilwa amesema Viongozi wa dini wanajukumu kubwa kuhakikisha wanakemea maovu hayo ya kikatili yanayoendslea katika jamii.
“Wachungaji, Masheikh, Mapadri, Maaskofu na viongozi wa dini wengine mnasikilizwa sana na makundi yote ndani ya jamii na ndiio maana Serikali inawategemea kutatua migogoro hata kwenye malezi.
” Hivyo ni muhimu mkichukua nafasi yenu kikamilifu jamii itajirekebisha na ukatili dhidi ya watoto na wanawake utakoma” alifafanua zaidi.
Amesema Wachungaji na Masheikh wana nafasi kubwa ya kurejesha jamii katika maadili mema kwa sababu wanasikilizwa na kuamimiwa na marika yote katika jamii.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Amani Mkoa wa Tanga Sheikh Juma Luwuchu amesema ni wajibu wa viongozi wa dini kushughulikia mmommonyoko wa maadili kwa sababu ni viashiria vinavyoonesha kwamba kizazi kijacho kitakuwa katika mazingira magumu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Viongozi wa Dini Mbali mbali nchini Mchungaji Thomas Muya amesema katika kuwajengea uwezo viongozi hao utatolewa mwongozo utakaowawezesha kutambua madhara na namna ya kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika katika Hoteli ya Dolphin Jijini Tanga una lengo ya kujadili mikakati ya kunusuru maovu na kuendeleza mema na nguvu kazi.
Mkutano huo umeratibiwa na Baraza la Viongozi wa Dini Mbali Mbaliv Tanzania ( IRCPT) na Taasisi ya Kimataifa Konrad Adenauer Stiftung(KAS).
Hata hivyo Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tanga, Gloria Maleo amesema asilimia 60 ya matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa vituo vya polisi yametendeka majumbani huku asilimia 40 yakifanyika shule mbalimbali.
Mwisho.