NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la vifo vya watu wanne wa familia moja ambao wamepoteza maisha baada ya kuvuta hewa chafu ya moshi kutoka kwenye jenereta.
Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro Jumanne leo Aprili 20, 2023 jijini Dar es Salaam amesema tukio hilo lilitokea Aprili 19, 2023 maeneo ya Temeke ambapo familia hiyo iliwasha jenerata ndani ya nyumba na baadae kulala.
“Majira ya saa 4 :00 usiku watu hao waliwasha jenereta baada ya umeme kuzimika na kuliweka ndani ya nyumba.”Amesema
Muliro amesema, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watu hao walipoteza maisha baada ya kuvuta hewa inayodaiwa kuwa ni hewa chafu ya moshi iliyokuwa inatoka kwenye jenereta baada ya kuwashwa.
Aidha, amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Kazija Mohamed (21), Munir Ibrahim (7), Munira Ibrahim (6) Muyyat Ibrahim (3).
Pia anesema Mume na Mke waliofahamika kwa majina ya Ibrahim Juma (28) na Aisha Ayubu (29) hali zao sio nzuri na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili