NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) Mhandisi John Nzulule ahakikishe ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Terminal 1 unakamilika haraka.
Pia amewataka viongozi na wafanyakazi wa TGFA wahakikishe wanashirikiana na mamlaka husika kuufanya uwanja huo wakati wote unakuwa nadhifu ili kukidhi hadhi ya viongozi wa kitaifa na kimataifa wanaoingia ama kuondoka nchini.
Pia amewaagiza Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete na Katibu Mkuu wa Utumishi, Juma Mkomi wafuatilie maslahi na motisha za watumishi wa taasisi hiyo ili kuinua ari yao ya utendaji kazi.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Jumanne, Machi 28, 2023 jijini Dar es salaam mara baada ya kufanya ukaguzi wa uwanja wa ndege wa Terminal 1.
Waziri Mkuu Majaliwa amekagua uwanja wa ndege wa Terminal I ili kujiridhisha na kazi ya ukarabati unaoendelea kwenye eneo la kuegesha na kufanyia matengenezo ya ndege za Serikali.
“Serikali ilishatoa kibali kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa karakana hiyo ambayo nimeelezwa itakapokamilika itawezesha kuegesha ndege kubwa mbili kwa wakati mmoja pale zinapohitaji matengenezo.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete amemweleza Waziri Mkuu kwamba Serikali ilitoa sh. bilioni 2.5 za ujenzi wa awamu ya kwanza ya ofisi za TGFA ambao umekamilika na ofisi zimeanza kutumika.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TGFA, amesema kukamilika kwa jengo hilo kumesaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa idara zilizopo uwanja wa ndege kwa kuwa lina nafasi za kutosha na mifumo ya kisasa kwa ajili ya marubani, wahandisi, wahudumu wa ndege na watumishi wengine.
Amesema awamu ya pili ya ujenzi inahusisha ujenzi wa eneo la kuegesha na kufanyia matengenezo ya ndege na inatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa sababu kibali cha ujenzi kimeshapatikana.
“Taratibu za kumpata mkandarasi zimeshakamilika na taratibu zote za kimkataba zimekamilika. Tunaahidi kusimamia kazi hii ili kupata thamani halisi ya fedha (value for money) katika mradi huu,” amesema.