
NA BENNY MWAIPAJA,BANGKOK,THAILAND
MAWAZIRI wa Fedha wa Tanzania na Burundi,Balozi Khamis Mussa Omar na Dk. Alain Ndikumana, kwa pamoja, wamekutana na wawakilishi wa Benki ya Dunia wakiongozwa na Makamu wa Rais anayehusika na Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dk. Ndiame Diop, kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa miundombinu wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor), unaolenga kubadilisha mtandao wa usafirishaji wa kikanda kuwa kichocheo muhimu cha ustawi wa kiuchumi katika ukanda huo.

[/caption
Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Omar amesema kuwa majadiliano hayo yalilenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka kuwa njia ya kawaida ya usafirishaji na kuwa eneo jumuishi la kiuchumi huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika maendeleo ya Reli ya Kisasa (SGR) ikiunganishwa na miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam, sambamba na uwekezaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.
[caption id="attachment_24727" align="alignnone" width="300"]
Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kulia), Waziri wa Fedha wa Burundi, Dk. Alain Ndikumana (kushoto) na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dk. Ndiame Diop, wakiteta jambo mara baada ya kufanya mkutano uliojadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa mradi mkakati wa miundombinu wa Ushoroba wa Kati (Central Corridor), unaolenga kubadilisha mtandao wa usafirishaji wa kikanda kuwa kichocheo muhimu cha ustawi wa kiuchumi kayika ukanda huo, wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Bangkok, nchini Thailand)
Alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa reli ya SGR iliyogawanywa vipande saba ambapo sehemu ya kwanza na ya pili, zinazounganisha Dar es Salaam na Dodoma imeanza kufanya kazi, huku kazi zikiendelea katika sehemu ya tatu hadi ya sita zitakazopanua mtandao wa reli kuelekea Tabora, Mwanza na hatimaye Kigoma, karibu na mpaka wa Burundi.
Aliongeza kuwa pamoja na umuhimu wa reli katika usafirishaji, ni lazima iunganishwe na mtandao wa barabara pamoja na vituo bora vya huduma za usafirishaji na ugavi na kwamba ushirikiano wa Benki ya Dunia na nchi za Tanzania, Burundi na DRC na washirika wengine wa maendeleo ni muhimu katika kufanikisha mradi huo.
Alisema lengo si kuondoa usafirishaji wa mizigo kwa malori na kutumia reli pekee, bali ni kujenga mfumo jumuishi wa usafirishaji ambapo malori yatapeleka mizigo kwenye reli, hatua itakayoongeza ufanisi, faida na uwezo wa miundombinu hiyo kuvutia uwekezaji na ufadhili.
Naye Waziri wa Fedha wa Burundi, Dk.Ndikumana alisema mradi huo unalenga kuboresha sekta ya kilimo nchini mwake na kurahisisha biashara ya usafirishaji wa bidhaa zinazopita nchini humo kwenda maeneo mengine, hatua itakayosaidia Burundi kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.
Alielezea umuhimu wa kimkakati wa kiungo cha reli, hasa kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya nikeli na kobalti eneo la Musongati, ambayo inakadiriwa kuwa kati ya tani milioni 150 na 230 zitazalishwa na kutumia ushoroba huo kuyafikia masoko ya kimataifa.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dk. Diop, alisema kuwa mradi huo ni muhimu katika kukuza biashara na ustawi wa watu katika Ushoroba huo na kuahidi kuwa Benki ya Dunia inaunga mkono mradi huo na iko tayari kuufanikisha.
Alisema kuwa Benki ya Dunia na washirika wa kikanda wanatarajia kufanya tathmini ya sekta binafsi ili kubaini fursa za uwekezaji na kuhakikisha kuwa miundombinu ya reli inaendana na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.
Kadri mradi huo unavyoendelea, makubalino ya wadau yapo wazi; kuwa Ushoroba wa Kati si mradi wa reli na miundombinu pekee, bali ni mpango wa muda mrefu wenye hatua mbalimbali unaolenga kuunganisha Bahari ya Hindi na maeneo ya ndani ya Bara la Afrika, kukuza biashara, kuzalisha ajira na kuimarisha maendeleo endelevu katika ukanda huo.





