NA MWANDISHI WETU, RIYADH,SAUDI ARABIA
. ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya
Kifalme ya Saudi Arabia zimesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU)
katika sekta ya nishati ambapo ushirikiano huo utahusisha pia kampuni
za mafuta, gesi na umeme katika nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yametiwa saini na Waziri wa Nishati, Dk Juma
Homera na Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, Waziri wa
Nishati wa Saudi Arabia pembezoni mwa Mkutano wa 25 wa WPC (25th WPC
Congress) unaoendelea jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Dk Homera amesema
suala hilo limewezekana baada ya wataalam wa pande zote mbili
kufanya kazi kwa ufanisi kwa muongozo na maelekezo ya Wakuu wa nchi
lengo likiwa ni kufungua ukurasa wa kushirikiana katika sekta ya
nishati ambayo nchi ya Saudi Arabia imepiga hatua kubwa.
Ametaja maeneo ambayo Tanzania na Saudi Arabia wamekubaliana
kushirikiana kuwa ni upatikanaji wa bidhaa za mafuta kupitia mikataba
ya kibiashara, uendelezaji wa miundombinu ya bidhaa za mafuta ikiwemo
ya usafirishaji na uhifadhi, tathmini ya fursa zitokanazo na mradi wa
LNG, kubadilishana ujuzi na utaalam katika eneo la utafutaji na
uendelezaji wa mafuta na gesi na kutafiti fursa za uendelezaji wa
viwanda vya bidhaa zitokanazo na mafuta na gesi (petrochemicals).
Maeneo mengine ya ushirikiano ni umeme na nishati jadidifu, kuchochea
ufanisi katika matumizi ya nishati, kubadilishana teknolojia na
suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo matumizi
ya nishati safi ya kupikia, biashara ya kaboni, kutafiti fursa
zinazohusiana na programu ya uendelevu wa nishati, matumizi ya akili
mnemba katika sekta ya nishati na mapinduzi ya kidijitali pamoja na
kujengeana uwezo na kubadilisha uzoefu katika sekta ya nishati kwa
ujumla.
Kwa upande wake, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, Waziri wa
Nishati wa Saudi Arabia amesema “utiaji saini wa makubaliano haya ni
zaidi ya kusaini karatasi, ni pambazuko la siku mpya inayoanza na
tumaini jipya lenye kuweka maslahi ya watu wa Tanzania na Saudi Arabia
katikati ya kila uamuzi kuhusu nishati, nchi zetu zimekuwa marafiki
kwa miaka mingi na sasa tunayo fursa ya kubadili urafiki huo kuwa
undugu kwa kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilisha
utaalamu, ujuzi na kushirikiana katika miradi ya maendeleo inayohusu
nishati”.
Hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo ilishuhudiwa pia na Balozi
wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhandisi Zena Ahmed Said pamoja na
wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC).
Caption
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (kulia) na Mwanamfalme
Abdulaziz bin Salman Al Saud, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia
(kushoto) wakiwa wameshika nyaraka za makubaliano ya ushirikiano
katika sekta ya nishati kati ya Tanzania na Saudi Arabia. Makubaliano
hayo yametiwa saini pembezoni mwa Mkutano wa 25 wa WPC (25th WPC
Congress) unaoendelea jijini Riyadh, Saudi Arabia.
—

