NA MWANDISHI WETU,KALAMBO,RUKWA
MJANE wa Hayati Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere leo Jumanne Oktoba 13 2026, amezindua rasmi Daraja la Maria Nyerere lililopo mto Kalambo katika barabara ya Kasitu-Nondo lenye thamani ya Sh.Bilioni 4.7 ambao limejengwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa daraja hilo, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Kalambo kwa kumpatia heshima ya kulizindua daraja ambalo limepewa jina lake, daraja ambalo limeimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kurahisisha mawasiliano na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI),Prof. Riziki Shemdoe, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha Sh.Bilioni 4.7 zitumike katika ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 80, kina cha mita 7 na upana wa mita 10.5 ambalo linalounganisha kata ya Sopa na Mpombwe katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
“Namshukuru Mhe. Rais kwa kuamua daraja hili liitwe jina la Mama Maria Nyerere na namshukuru sana Mama Maria Nyerere kwa kukubali daraja hili liitwe jina lake pamoja na kukubali ombi la kuja kulizindua rasmi, ili kuchochea uchumi na kufungua fursa kwa wananchi wa Kalambo na nchi jirani hususan katika shughuli za usafiri na usafirishaji,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kalambo Edfonce Kanoni amesema daraja hilo ni kiungo cha uchumi katika Jimbo la Kalambo kwani kutoka lilipo ukitembea kilomita 22 linawaunganisha wananchi na fursa ya mpaka wa Zambia ambao una maporoko makubwa ya Kalambo Falls ya kihistoria yenye urefu wa mita 200 kutoka juu, hivyo litachochea uchumi lakini ni fursa kwa wananchi wa nchi hiyo jirani kulitumia kiuchumi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasitu John Sizo amempongeza Rais kwa kuwezesha ujenzi wa daraja hilo, ambalo kabla ya kujengwa lilikuwa ni chanzo cha vifo vya wananchi wa kijiji chake na kuongeza kuwa, anashukuru ujenzi wa daraja hilo limewawezesha kumuona Mama Maria Nyerere, Mke wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Diwani wa Kata ya Mpombwe Paulo Kasitu amesema, daraja hilo limekuwa ni mkombozi wa kata za kata ya Sopa na Mpombwe kwani kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo wamepoteza akina mama wengi sana na kuongeza kuwa binafsi ameshuhudia vifo kwa akina mama wapatao saba.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kalambo Leopard Mbita amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumleta Mama Maria Nyerere Kalambo na hatimaye kuwapatia fursa wananchi kumshuhudia mama ambaye ni chanzo cha taifa kuishi kwa Amani kutokana ushauri mzuri aliokuwa akimpatia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Daraja hilo lililozinduliwa leo, lilipewa jina la Maria Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Rukwa mwaka 2024.















