NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UTATA umegubika kufuatia tukio la mwanafunzi wa shule ya msingi Olympio ya jijini Dar es salaam kudaiwa kuchapwa viboko na mwalimu wake hadi kupasuka jicho.
Taarifa za mtoto huyo kupasuliwa jicho, zimetolewa na ndugu wa familia ya Mama mzazi wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Aisha Sijavala (jina limehifadhiwa)ambaye amesema, tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki iliyopita
“Olympio wanapiga sana watoto. Mwalimu kampiga mtoto Aisha Kijavala kampasua jicho juzi wamehangaika Mwananyamala Hospitali ambapo februari 23, 2023 wamemhamishia Muhimbili na februari 24, 2023 wamemuingiza chumba cha upasuaji)! Ndio wote wako hapo hospitali duh jamani,” kimeeleza chanzo hicho cha taarifa.
Kwa mujibu wa mmoja wa walimu ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa sio mzungumzaji , tukio hilo ni la kweli lakini mazingira yanayotajwa sio ya kweli.
“Hakupasuliwa jicho hizi ni taarifa za uongo wakati mwanafunzi anachapwa, kuna kijiti kiliruka na kumgusa upande wa jicho ni eneo dogo na mtoto aliwekewa dawa anaendelea na masomo,” amesema mwalimu huyo
Kwa upande wake, Sijavala mama mzazi wa mtoto huyo akizungumza kwa simu na Mwananchi alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Tulishamalizana na mwalimu, tukio limetokea kwa bahati mbaya. Nipo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) (ilikuwa jana (juzi) asubuhi) chumba cha upasuaji siruhusiwi kuongea na simu,” amesema.
Hata hivyo, Ofisa Elimu msingi wilaya ya Ilala, Sipora Tenga amekanusha taarifa za mtoto huyo kupasualiwa jicho.
Japo tukio hilo la mwanafunzi wa shule hiyo kudaiwa kupasuliwa jicho limekuwa na danadana, tukio hilo ni mwendelezo wa matukio yanayoendelea kuwakumba wanafunzi ambapo Januari 10 mwaka huu, ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera,Isaya Emmanuel aliyeonekana akiwachapa viboko kwenye nyayo wanafunzi wawili wa darasa la nne waliokuwa wakilia.
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alitoa ufafanuzi wa tukio hilo la mwalimu mkuu huyo kuwaadhibu watoto hao wawili isivyostahili, huku akisema kuwa alishushwa cheo na kusimamishwa kazi.
Pia mwaka mwaka 2018 mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera alifariki baada ya kuchapwa viboko na mwalimu wake, kwa madai ya kuiba pochi yake.
Mwendelezo wa kukithiri kwa matukio ya wanafunzi kuadhibiwa vikali na walimu wao, unabainishwa katika utafiti wa Shirika la HakiElimu wa mwaka 2020.
Kulingana na utafiti huo, asilimia 87.9 ya watoto shuleni waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90 kati ya hao, wakisema walifanyiwa ukatili kwa kupewa adhabu za viboko zinazotolewa shuleni.