NA WAANDISHI WETU, RUVUMA
WATAKAOKIDHI vigezo vya kujenga vituo vidogo vya mafuta kuanzia sasa watawezeshwa na serikali kupata mikopo ya Sh.Milioni 75 na riba ya asilimia tano ambapo marejesho yake ni hadi kipindi cha miaka saba
Mikopo hiyo itatolewa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikiwa ni dhamira Serikali kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu vya bidhaa za mafuta (Dizeli na Petroli) maeneo ya vijijini ili kuondoa njia zisizo salama za uhifadhi wa mafuta hayo.
Akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo,Mhandisi Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo wakati akitoa semina kwa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma, Oktoba 5 mwaka huu kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga. alieleza mambo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa ujenzi wa vituo hivyo kwa wale watakaokidhi vigezo na kupata mkopo wa kuvijenga.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, Mwongozo huo unaainisha bayana vigezo kwa mwombaji wa mkopo ambavyo vimegawanyika katika makundi mawili; kiufundi na kifedha.
Mhandisi Tarimo alivitaja baadhi ya vigezo vya kiufundi kwa mwombaji kuwa ni pamoja na mtu binafsi au kikundi cha wajasiriamali kijijini kilichosajiliwa na Mamlaka husika au Serikali ya kijiji kuwa na kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Kigezo kingine ni mwombaji kuwasilisha kwa REA barua ya maombi ya mkopo wa ujenzi wa kituo au vituo vipya tu na siyo vinavyohitaji ukarabati au vilivyoanza kujengwa.
Aidha, mwombaji atatakiwa kuwa na barua ya uthibitisho kutoka Halmashauri ya kijiji na Wilaya inayomruhusu kuendesha biashara ya kituo cha mafuta katika eneo aliloomba pamoja na kuwa na namba ya mlipa kodi (TIN Namba) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzani
Pia, alieleza kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na uthibitisho wa umiliki wa ardhi (Hati Miliki ya ardhi au Hati za kimila au uthibitisho wa umiliki wa ardhi) kutoka kwa Halmashauri ya Kijiji au Wilaya na kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka husika pamoja na kujaza fomu ya kuonesha namna anavyokusudia kufanya biashara ya mafuta.