NA DANSON KAIJAGE,DODOMA
UMOJA wa Friends Of Mshehereshaji Mwangata Assosiation (FOMMA) umetoa baiskeli inayotembea ambayo hutumiwa na watu wenye ulemavu kwa mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) Jackson Shalua aliyewahi kuwa kuwa Mkuu wa Jimbo la Makao Makuu,aliyepatwa na tatizo la uvimbe mgongoni mwaka 2010 na kufanyiwa upasuaji mwaka 2015 ambapo alipata shida ya kushindwa kutembea kutokana na matatizo ya kiafya.
FOMMA imetoa baiskeli hiyo kwa mchungaji mstaafu Shalua ambaye alilitumikia Kanisa hilo hadi kustaafu lakini baada ya kupata tatizo la ugonjwa wa kushindwa kutembea kutokana na tatizo la mgongo na kufanyiwa upasuaji hakuweza kupata msaada kwa haraka.
Akizungumza katika hafla fupi ya kumkabidhi baiskeli hiyo kwa mchungaji huyo jana 2023,Mwenyekiti wa Umoja huo,Dk.Gasper Kisenga alisema kuwa chini ya mbeba maono wa taasisi hiyo ajulikanaye kwa jina la MC Mwangata umoja huo ulikubaliana kuhakikisha unatoa sadaka ili kumwezesha mchungaji Shalua ili naye apate nyenzo muhimu ya kusafiria.
Kwa upande wake Mchungaji Shalua alisema kuwa alianza kupata shida ya uvimbe mgongoni tangu mwaka 2010 na kufanyiwa upasuaji mwaka 2015 ambapo ndipo tatizo la kupoteza nguvu za kutembea lilipoanza.
Aidha alisema katika kuendelea na matibabu hali yake haikuweza kutengamaa licha ya kuwa alitengeneza kiti cha kutembea ambacho hakikuwa na kiwango lakini kutokana na kupata kiti kinachotembea ambacho ni cha kisasa tayari anaweza kutembea umbali mrefu kwa kupata huduma ikiwa ni pamoja nankupata wepesi wa kwenda ibadani.
Naye mbeba maono wa Umoja huo MC Mwangata alisema kutokana na maono yake ya kuwajali wahitaji alianzisha umoja huo kwa kuwaomba watu wote wenye moyo wa kusaidia wahitaji kumuunga mkono bila kujali itikadi za dini,kabila,siasa wala kipato cha mtu.
MC Mwangata alisema kuwa kwa muda wa miaka minne sasa wamewafikia wahitaji mbalimbali ikiwemo shule kongwe ya watu wasioona Buigiri wilayani Chamwino,mkoani Dodoma,Kondoa na jana FOMMA licha ya kumpatia Mchungaji mstaafu kiti kinachotembea wameweza kupeleka misaada kwa walemavu wa ngozi (Albino) na misàda mbalimbali kwenye hospitali ya rufaa ya Dodoma kwenye wodi ya watoto wenye magonjwa mbalimbali hususani wenye utapia mlo.
Kwa upande wa waliopokea misaada akiwemo Amina Alphani ambaye anatokea kwenye familia ya watoto 8 huku kati ya watoto watano wakiwa albino alisema anashukuru kwa kukumbukwa na FOMMA kwa nia ya kupatiwa misaada mbalimbali kwani kwao mahitaji ni gharama zaidi.
Naye Hellen Alex Muuguzi wodi ya watoto katika hospitali ya rufaa ya Dodoma,alisema walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwapatia lishe watoto hususani wenye utapia mlo.




