NA FARIDA RAMADHANI, WFM, DODOMA
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango na ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kujadili namna ya kushughulikia athari za upungufu wa dola za Kimarekani katika mzunguko wa fedha ili kunusuru uchumi wa nchi zinazoendelea.
Dk Nchemba ametoa maagizo hayo wakati wa kufungua kikao kilichowashirikisha wataalam kutoka Shirika la Fedha na Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya Programu ya Huduma za Mikopo (EFC), kwa kushirikiana na wataalam wa ndani wa Serikali.
Alisema mabadiliko ya Sera za Fedha nchini Marekani ya kubana matumzi na kupunguza dola kwenye mzunguko wa fedha, yameleta athari zinazoonekana mpaka kwenye nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tumekuwa tukirejea Uviko na vita baina ya Urusi na Ukraini kama moja ya vitu vinavyoathiri uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lakini upungufu wa dola unaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa ikiwemo uagizaji wa mafuta na uagizwaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika katika shughuli za Sekta Binafsi”, amesema Dk.Nchemba.
Amesema ni vema kutafuta namna ya kushughulikia jambo hilo kisera ili kunusuru nchi zinazoendelea kwa kuwa sekta ya nje ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Harris Tsangaride, amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kiuchumi na kijamii.
Amepongeza Serikali kwa Sera zake nzuri ambazo zinaendelea kutekelezwa katika kukabiliana na athari za vita ya Ukraine na kuongeza kuwa ni matarajio yao kuwa zitaendelea kuchokea ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi.
Tsangaride amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika kanda ambazo zinafanya vizuri katika kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana na Shirika hilo na hivyo katika kikao hicho watajadiliana namna bora ya kuendelea kuiona nchi ikifanya vizuri zaidi.