NA MWANDISHI WETU, KATAVI
UKOSEFU wa ajira kwa wenye sifa, vikwazo katika huduma bora za Afya, elimu kutokufanywa kama nyenzo ya ukombozi pamoja na kukithiri kwa umasikini uliopitiliza ni miongoni kwa changamoto zinazowakabili watanzania
Aidha changamoto nyingine ni hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa gharama kubwa za maisha
Vilevile , Kilimo kutokupewa nafasi kubwa kwenye mipango ya nchi licha ya kuajiri asilimia 67 ya wananchi ni miongoni mwa changamoto
Hayo yametajwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo Juma Duni Haji, wakati akizungumza na wananchi wa Mpanda mkoani Katavi akiwa katika muendelezo wa ziara ya kutambulisha ahadi za chama.
Duni amesema,ACT Wazalendo imefanya utafiti na kujiridhisha kuhusiana na masuala hayo matano kuwa ni mambo yanayowasumbua watanzania na serikali imekosa mbinu sahihi za kuwanasua
Amesema ni wakati muafaka sasa na kwa watanzania kuachana na Chama Cha Mapinduzi(CCM),Kwa kuwa katika miaka zaidi ya 60 ya uhuru imeshindwa kutatua vikwazo hivyo.
“Sisi ACT tukishasema mkitupa ridhaa tutaenda kufanya mapinduzi katika Kilimo ambacho kinaajiri asilimia 67 ya watanzania na tunafahamu tukileta Mapinduzi kwenye Kilimo tutakuwa tumepiga hatua kubwa juu ya kuyaondoa masuala hayo yanayowasumbua watanzania”amesema Duni.
Aidha chama hicho kimesema Serikali inatakiwa kutenga fedha ya kutosha kwa ajili ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) iweze kununua mazao.
Mwenyekiti alisema chama hicho kilifanya utafiti na kubaini robotatu ya watanzania hasa wa mjini kilio kikubwa ni gharama za maisha kuwa kubwa zikichangiwa na bei za vyakula.
“Tunataka NFRA iwe na uwezo wa kuweka chakula mpaka tani milion tatu za mahindi, mpunga, uwele mtama na maharage kuwa na chakula cha akiba ambacho ikitokea lolote Watanzania hawawezi kukumbwa na njaa angalau miezi mitatu” amesema.
Kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe ameeleza kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika mkoa wa Katavi kati ya Halmashauri na wananchi na Wananchi na Hifadhi.
Ameeleza chanzo cha migogoro kuwa ni kutokana na kasi ndogo ya upangaji wa miji na kukosekana kwa eneo la kutosha la malisho.
Zitto ameeleza sababu nyingine za migogoro hiyo kuwa ni kutokana na ardhi kuwa chanzo cha mapato ya Halmashauri .
Makamu Mwenyekiti Bara Dorothy Semu alisema mahitaji muhimu kama elimu afya na maji bado ni bado havipatikani kwa uhakika kwa wananchi huku wananchi wakiandamwa na umasikini na kushindwa kumudu kununua baadhi ya mahitaji.