NA MWANDISHI WETU, TANGA
WILAYA ya Mkinga imepokea Sh.Bilioni 1 na Milioni 350 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya sekta ya elimu Mradi wa BOOST.
Miundombinu inajumuisha ujenzi wa madarasa 32, nyumba 6 za walimu, matundu 42 ya vyoo pamoja na ofisi za walimu.
Sambamba na hilo itajengwa shule mpya moja ya msingi ambayo itakuwa na mkondo mmoja katika kijiji cha Maramba B wilayani humo.
Akikagua ujenzi wa Shule ya Msingi Mtimbani, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu alisisitiza waratibu wa ujenzi huo kukamilisha mradi huo kwa muda waliopewa na kwa ubora unaotakiwa na TAMISEMI.
Surumbu alitoa maelekezo hayo kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ofisa Elimu Msingi Wilaya Mwalimu Omari Mashaka baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi huo unaoendelea katika hatua ya uchimbaji wa msingi.
“Hakikisheni mnapita mara kwa mara kusimamia ujenzi, sitapenda kusikia mradi umechelewa kukamilika, wala sitapenda kuona madarasa yanajengwa chini ya viwango, zingatieni vipimo vyote vilivyopo katika ramani.”
Amesisitiza zaidi kuwa fedha aliyoleta Rais Dk. Samia Suluhu Hassan lazima isimamiwe vizuri ipasavyo na isipotee hata tone.
Aidha Surumbu amewaomba wananchi kushiriki kutoa nguvu kazi katika miradi yote ya ujenzi inayoendelea kwenye shule mbalimbali Wilayani humo.