NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Can Tanzania limeahidi kuchangia jumla ya Sh milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kupitia Taasisi ya Revival Education Trust iliyochini ya Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, kwa lengo la kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye changamoto za kiuchumi kupata fursa ya elimu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 20 ya wanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Huria Ukonga Skillful, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Sixbert Mwanga amesema elimu imekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya maisha na mafanikio aliyoyapata, hivyo anaona umuhimu wa kuunga mkono juhudi kwa kuwasaidia wanafunzi wanaokabiliwa na vikwazo vya kiuchumi.
Amesema katika safari yake ya elimu, alikumbana na changamoto ambazo zilimfanya atambue umuhimu wa kupata msaada, akibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hukosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu za kifamilia, hata pale wanapokuwa na uwezo wa kufanya vizuri kitaaluma.
Mwanga amesema wapo wanafunzi ambao hushindwa kuendelea na masomo baada ya kutofaulu mitihani au kukosa uwezo wa kugharamia elimu, huku wengine wakipata nafasi ya kuendelea kutokana na msaada wa wazazi, ndugu au watu wengine wenye uwezo wa kifedha.
“Wengine walipomaliza darasa la saba walipata nafasi ya kwenda sekondari, lakini wapo ambao hawakupata nafasi hiyo. Hata kama hawakufaulu, wengine walisaidiwa na wazazi au ndugu zao kuendelea na masomo, lakini sisi hatukupata nafasi hiyo,” amesema Mwanga
Aidha, amesema pamoja na ahadi ya kuchangia Sh milioni mbili kila mwaka kwa miaka mitano, yuko tayari kushirikiana na Revival Education Trust katika kuimarisha taasisi hiyo ili iweze kupanua wigo wa shughuli zake na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji.
Ameongeza kuwa uzoefu alioupata katika kuanzisha na kuendesha taasisi mbalimbali umemfundisha umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya kisheria na kiutawala ili kuhakikisha taasisi zinafanya kazi kwa uwazi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye Muasisi wa Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, Diodorus Tabaro amesema limepanga kuwasaidia wanafunzi 100 kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi kurejea shuleni mwaka ujao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Amesema kati ya wanafunzi 100 watakaonufaika na mpango huo, 50 watapata nafasi za bweni, huku wengine 50 wakisoma bila kulala shuleni, ili kuwawezesha kuendelea na masomo kulingana na mazingira yao.
Tabaro ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo ya kufungua milango ya elimu kwa watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji, akisisitiza kuwa changamoto za kiuchumi hazipaswi kuwa kikwazo cha kutotimiza ndoto za watoto.







