NA FARIDA RAMADHANI,WF,DODOMA

SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake, wajasiriamali na wananchi wa vijijini

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025.
Munde alisema kuwa lengo ni kuhakikisha bima inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania, kwa kuwa na uelewa wa umuhimu wake, namna ya kupata huduma na taratibu za kudai fidia wanapokumbwa na majanga mbalimbali.

“Elimu hiyo isiishie mijini pekee. Iwafikie wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake, waendesha pikipiki na bajaji, wafanyakazi, wajasiriamali na wananchi wa maeneo ya vijijini. Tunataka kuona bima inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania”, alisisitiza Munde.

Naibu Waziri wa Fedha,Mhandisi Ali Mshamu Munde akimkabidhi Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Prof. Abel Makubi , mfano wa hundi ya Sh.Milioni 221 iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na wadau wake katika Sekta hiyo, kwa ajili ya kusaidia huduma ya upandikizaji uloto kwa watoto wenye mahitaji ya huduma hiyo, katika hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025, jijini Dodoma.
Alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima ili kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo kwasababu sehemu kubwa ya wananchi bado hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa bima, namna ya kupata huduma za bima na namna ya kufuata taratibu za kudai fidia.

Aidha, Munde alisisitiza umuhimu wa sekta ya bima katika kufanikisha azma ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance – UHI), kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya masuala ya afya pamoja na taasisi nyingine zinazohusika ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na kinga ya afya.

“Serikali inaendelea kuweka mkazo mkubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazopatikana kwa wote. Katika kutekeleza azma hii, Bima ya Afya kwa Wote ni eneo muhimu sana. Sekta ya bima ina nafasi kubwa katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata ulinzi wa afya zao kwa gharama nafuu” alisema Munde.

Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa maslahi ya wateja wa huduma za bima yanalindwa na mwenendo wa watoa huduma wa bima unasimamiwa kwa weledi na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Meza kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Wizara ya Fedha katika Hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025, jijini Dodoma.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa sekta ya bima iliyo jumuishi na inayochangia katika maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Hamad Bakar Hamad alisema Sekta ya bima nchini ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa Taifa, kulinda wananchi dhidi ya vihatarishi mbalimbali na kuchochea uwekezaji kupitia ukusanyaji wa rasilimali za muda mrefu.
Alisema ni muhimu kwa TIRA kuongeza juhudi za kupanua wigo wa huduma za bima, ikiwemo matumizi ya huduma za bima kupitia benki (bancassurance), bima ya Kiislamu (Takaful) na majukwaa ya kidijitali, ili kuongeza upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi.
Aidha,Hamad aliisisitiza TIRA na watoa huduma za bima kuimarisha matumizi ya teknolojia katika usajili, uuzaji wa bima, malipo na ulipaji wa madai ili kuongeza uwazi, kudhibiti udanganyifu na kuwafikia wananchi wengi zaidi huku akitilia mkazo kuwa maendeleo ya kidijitali yanapaswa kuambatana na ulinzi wa taarifa za wateja, usalama wa mifumo na uzingatiaji wa sheria na kanuni husika.
Awali, akitoa maelezo ya mwenendo wa Sekta ya Bima nchini, Kamishna wa Bima Tanzania, Dk. Baghayo Saqware, alisema Soko la bima nchini limeendelea kukua kwa kasi katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, likichangia kuimarisha uchumi na kuongeza fursa za ajira.
Alisema ukuaji huo umechangiwa na upanuzi wa huduma za bima, kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima na juhudi za wadau katika kuboresha huduma.
Dk. Saqware alibainisha kuwa ajira katika sekta hiyo ziliongezeka kutoka takribani 3,000 hadi kufikia 6,474, huku ada za bima zilizokusanywa zikiongezeka kutoka Shilingi bilioni 824.3 mwaka 2020 hadi Shilingi trilioni 1.015 mwaka 2024.
Mafanikio hayo yanaonesha sekta ya bima inayozidi kuimarika katika kukuza shughuli za kiuchumi na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.
Aidha, matumizi ya huduma za bima yameendelea kuongezeka, hali inayoashiria kuimarika kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujikinga dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha hasara za kifedha.
Vilevile, Dk. Saqware alisema kuwa Sekta ya Bima imeendelea kuchangia ustawi wa wananchi kupitia ulipaji wa madai na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.



