NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima(TIRA) Dk.Baghayo Saqware ametoa onyo juu ya dhuluma wateja kwenye ulipaji fidia za madai ya bima.

Dk.Saqware amesisitiza kuwa mteja yeyote asidhulumiwe na anapaswa kulipwa madai yake kwa wakati.
Aidha amesema kila mtu anatakiwa kulipwa kile anachostahili na asionewe kwenye suala zima la malipo kwa sababu ni mchangiaji.

Kamishna Dk.Saqware ameyasema haya leo Jumatatu Agosti 18,2025 katika mkutano baina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na TIRA uliofanyika jijini Dar ES Salaam kueleza mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Dk.Sqware amesema malalamiko ni mengi lakini hakuna budi malalamiko hayo kufanyiwa kazi ili kusiwepo na yeyote atakayedhulumiwa.

” Naagiza mteja yeyote wa bima asidhulumiwe,kila mtu alipwe madai yake kwa wakati,kila mtu alipwe anachostahili na kusiwe na kuonewa kwenye malipo ya fidia” amesisitiza.
Akielezea juu ya Mpango wa Bima ya Afya kwa wote Kamishna Dk.Saqware amesema mpango huo una manufaa makubwa kwa watanzania na umeshaanza tangu Januari Mosi, mwaka huu.

Amesema gharama ya Mpango huo bado haujatajwa ni kiasi gani cha fedha lakini itatangazwa na Waziri mwenye dhamana hapo baadaye.
Wakati huo huo Kamishna Dk. Saqware ametangaza fursa kwa watanzania wanaohitaji kuwa Mawakala wa Mpango wa Bima kwa afya kuwa milango ipo wazi na vigezo na masharti yake ni nafuu sana.
“Ili kuwa Wakala tembelea tovuti ya
https://tiramis.tira.go.tz vigezo na masharti vipo pale hivyo natoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa hii ya kiuchumi” amebainisha

Akielezea mafanikio ya TIRA Dk. Saqware amesema, wanufaika wa huduma za bima nchini wameongezeka kutoka milioni 14 mwaka 2021 hadi milioni 25.9,mwaka huu huku hamasa ikiendelea ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.

Pia, amesema mali na mitaji katika soko la bima imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.2 mwaka 2021 hadi trilioni 2.3,mwaka huu.
“Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji mzuri wa sera chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dk.Samia Suluhu Hassan na mafanikio haya yapo kitakwimu zaidi.”
Amesema, pia mafanikio hayo yanatokana na hamasa na elimu inayotolewa na mamlaka kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari nchini.
Vilevile, Dk.Saqware amesema, idadi ya watoa huduma imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,425 mwaka huu ambapo kuna ongezeko la watoa huduma mpya ikiwemo afya, kidijitali, na bima mtawanyo kutoka moja hadi nne.
Pamoja na mambo mengine Kamishna Dk.Saqware amesema kuna ongezeko la kampuni za bima kutoka 32 mwaka 2021 hadi kampuni 35 huku wawekezaji wengi wakivutiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.
“Serikali imefanikiwa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na kanuni zake.
“Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya 2023 inatoa nafasi kaa wananchi kupata huduma za afya kwa wingi na sahihi, na sheria hii inaenda kuongeza watumiaji wa huduma za afya, kuboresha maisha ya wananchi hasa watakapopata kadi za afya. Aidha, sheria hiyo inatoa nafasi NHIF kuwa chini ya uangalizi wa TIRA.”
Amesema Serikali imefanikiwa kufanya maboresho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022. Serikali iliona ni muhimu kwa miradi yake inayotekelezwa nchini kuwa inakatiwa bima ili kuilinda pamoja na miundombinu.
Katika hatua nyingine, amesema wamefanikiwa kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA kutokana na maelekezo ya Rais Dk.Samia ambapo mamlaka imepiga hatua kubwa na imeweza kuunganisha mfumo wake na Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, LATRA,TASAC na NIDA.
“Matarajio ni kuunganisha taasisi zaidi ya 30 bara na visiwani ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi.”
Kupitia kikao kazi hicho, TIRA imebainisha kwa kina mafanikio yake, ilipotoka,ilipo na inapoelekea
“Pili niishukuru sana Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa dhati kabisa wamekuwa wasimamizi wazuri kwetu.”
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), chini ya Sheria ya Bima, Sura ya 394 ina jukumu la kuendeleza sekta ya bima Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, ni taasisi ya Serikali ilioanzishwa ili kutekeleza majukumu ya kusimamia soko na kuendeleza biashara ya bima nchini na masuala yanayohusiana na bima kwa mujibu wa sheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu mengine ni kusajili kampuni za bima nchini, kusimamia na kukagua mwenendo wa kampuni za bima nchini, kutoa elimu ya bima kwa umma, kuhakikisha uendelevu, uhimilivu na usalama wa soko la bima nchini. Vilevile, kuishauri Serikali kuhusu masuala ya bima hapa nchini.

