NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Madini la Taifa limewaasa Wachimbaji wa Madini kuachana na dhana potofu ya ushirikina kwa kuwa madini ni sayansi inayofanya kazi kitaaluma.
Aidha limewataka wachimbaji kutorubuniwa na Waganga wa Kienyeji kwa kupeleka wanyama kama kuku na mbuzi wakiaminishwa kwamba watapata madini
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Stamico Venance Mwasse katika kikao kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar as salaam leo Ijumaa Oktoba 16,2026.
” Uchimbaji madini ni sayansi inaayofanya kazi kitaaluma hivyo mambo ya kutuchinjia shingo za kuku na kutumalizia kuku ikifika Desemba tukose vitoweo hebu wachimbaji tutoke huko” amesema Mwasse
Amesisitiza kuwa ifike mahali wachimbaji watumie njia za kitaalamu katika uchimbaji madini na sio imani potofu zilizopo hivi sasa miongoni mwa wachimbaji wengi
Wakati huo huo Mwasse ameeleza kuhusu mafanikio ya Shirika hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 1972 na kusisitiza kwamba Stamico imepitia vipindi mbalimbali vya kusimama na kuanguka hadi sasa.
Amesema Stamico ilipita katika kipindi kigumu cha kuanguka mwaka 1997 hadi 2019 ambapo serikali ilifikiria kuifuta kabisa lakini badala yake ikawa ndio mwanzo mpya wa Shirika hilo.
” Tulifikia hatua ya Stamico kuwa ICU lakini tuliamua kufuata R mbili ( Reform and Rebuild)Kati ya nne za Mheshimiwa Rais,Dk.Samia Suluhu Hassan ambazo ni kujenga upya na kufanya mageuzi ndizo zilizotufikisha hapa leo hii”amesisitiza Mwasse.
Amesema kutoka makusanyo ya mapato ya Sh.Bilioni 1.3 hadi Trilioni 147.8 ni hatua kubwa sana kwa Shirika lililokuwa linaelekea kufa.
Sambamba na ongezeko hilo la mapato,Stamico imefikia hatua ya kujilipa mishahara wao wenyewe na kutoa gawio la Sh.Bilioni 11 kwa Serikali
“Ni mafanikio makubwa sana kwetu sisi Stamico kujilipa mishahara sisi wenyewe pasipo kuitegemea serikali,na tunajilipa mishahara kutokana na makusanyo tunayokusanya” amejinasibu Mkurugenzi huyo.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya rasilimali watu kutoka 100 hadi 800.
Aidha Stamico inajivunia kufanya uwekezaji kwenye viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha chumvi kilichopo mkoani Lindi na kiwanda kikubwa cha kutengeneza nishati safi kitakachozinduliwa hivi karibuni mkoani Dodoma.
Mbali na hayo Stamico kwa kushirikiana na wadau ipo mbioni kuanzisha benki ya wachimbaji kwaajili ya kuwawezesha kupata mikopo Kwa haraka na uhakika zaidi.
Pamoja na mambo mengine Stamico inajivunia kuwa na masoko 44 ya madini na vituo vidogo 120 Tanzania nzima.
Mwasse amekazia kuwa Stamico itaendelea kutimiza najukumu yake hususani kwenye eneo ka utafiti,ushauri wa kitaalamu kwa wachimbaji ,biashara,ya uchorongaji madini,uchenjuaji na walezi kwa wachimbaji wadogo kama inavyoelekeza sura ya 123.







