NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya mawasiliano ya simu, redio, posta na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kupunguza pengo la mawasiliano na kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wa vijijini na mijini nchini.
Akizungumza katika Kikao Kazi baina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam leo Jumanne Novemba 3,2026 Mkurugenzi wa Uendeshaji,Utafiti na Maendeleo wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema mfuko huo umeendelea kupanua miundombinu ya mawasiliano kupitia ujenzi wa minara ya simu, uboreshaji wa vituo vya redio, usambazaji wa vifaa vya TEHAMA shuleni na uanzishaji wa vituo vya intaneti ya bure katika maeneo mbalimbali.
Katika sekta ya mawasiliano ya simu, Mhandisi Richard ameeleza kuwa kati ya minara 2,324 iliyopangwa kujengwa katika awamu mbalimbali, minara 2,199 imejengwa.
Aidha amesema minara 758 iliyojengwa kupitia mradi maalumu imewashwa yote, na kunufaisha kata 713, vijiji 1,401 na wananchi takribani milioni 8.5.
“Utekelezaji wa Awamu ya 10, inayohusisha ujenzi wa minara 287 kwa gharama ya sh.bilioni 29, unaendelea. Hadi wakati wa kuandaliwa kwa taarifa hiyo, minara 65 ilikuwa imewashwa, sawa na asilimia 23.
Katika sekta ya utangazaji, UCSAF imekamilisha ujenzi wa vituo 11 vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC) kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5. Miradi mingine 26 ya vituo vya redio inaendelea, na kufanya jumla ya vituo vilivyojumuishwa katika mpango huo kufikia 37.” amefafanua Mhandisi huyo
Kwa upande wa redio za jamii, Mhandisi Richard amebainisha kuwa ,mfuko huo umewezesha kukamilika kwa studio tano na minara saba ya redio za jamii kwa gharama ya takribani Sh.Bilioni 5.7. Miradi mingine 15 inaendelea kutekelezwa kwa gharama ya takribani Sh.Bilioni 6.46.
Kadhalika Mhandisi Richard amefafanua kuwa katika sekta ya elimu, UCSAF imewezesha shule za umma 1,167 kupata vifaa vya TEHAMA na maabara, huku Serikali ikiwa imewekeza Sh.Bilioni 17.7 katika mradi huo hadi Oktoba 2026.
Aidha amesema kwamba ,shule 22 zinazohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu zimepatiwa vifaa vinavyowasaidia kujifunza, vikiwemo mashine za nukta nundu, kompyuta mpakato, vifaa vya kusoma kidijitali na vifaa vya kukuza maandishi. Serikali imewekeza shilingi bilioni 1.84 katika mradi huo hadi Juni 2025.
Katika hatua nyingine ,Mhandisi Richard amesema katika kuimarisha ujuzi wa kidijitali, walimu 5,094 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamenufaika na mafunzo ya TEHAMA tangu mwaka wa fedha 2016/2017.
Wakati huohuo, Mhandisi huyo ametanabaisha kuwa ,wanafunzi wa kike 1,581 wamejengewa uwezo kupitia mpango wa Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA.
“Vilevile, UCSAF inaendelea kusambaza huduma za intaneti ya bure katika maeneo ya wazi yenye watumiaji wengi. Miongoni mwa maeneo yaliyofikiwa ni viwanja vya maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Nyerere Square jijini Dodoma na Soko la Nyamagana jijini Mwanza.” amesema bayana Mhandisi Richard.
Katika sekta ya posta, Mhandisi huyo ameeleza ameeleza kuwa mfuko huo umeendelea kuunga mkono Shirika la Posta Tanzania kwa kutoa vifaa vya kisasa, vikiwemo kompyuta, vifaa vya kusaidia utoaji wa huduma kidijitali, printa na mashine za kunakili nyaraka ili kuboresha ufanisi wa huduma.
Pamoja na mafanikio hayo,Mhandisi Richard smejinasibu kuwa baadhi ya miradi bado iko katika hatua za ujenzi, manunuzi na ukamilishaji wa mikataba. UCSAF itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara.
“Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuchochea uchumi wa kidijitali, kuboresha upatikanaji wa taarifa na elimu, na kuongeza fursa za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi nchini.” amehitimisha Mhandisi Richard.










