NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, huku nchi hizo zikikubaliana pia kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi kutafuta fursa za ushirikiano.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Angola, João Lourenço, Rais Samia amesema licha ya nchi hizo kuwa na uhusiano mzuri wa muda mrefu, kiwango cha biashara kati yao bado ni kidogo na kinahitaji kuimarishwa.
Amesema katika kutekeleza uamuzi wa kufungua tena ubalozi huo, Tanzania itateua Balozi atakayesaidia kuratibu na kusimamia masuala ya ushirikiano kati ya nchi hizo.
Ameeleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Angola ulijengwa na viongozi wa awali wa mataifa hayo, wakiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa kwanza wa Angola, Hayati Dk. Agostinho Neto, ambao walishirikiana katika harakati za ukombozi wa Angola hadi ilipopata uhuru mwaka 1975.
Rais Samia amesema viongozi waliofuata wameendelea kuimarisha uhusiano huo, akimpongeza Rais Lourenço kwa juhudi zake za kuendeleza ushirikiano kati ya mataifa hayo.
Aidha, amesema hatua zilizochukuliwa na Rais Lourenço, ikiwemo mwaliko wa ziara ya kitaifa nchini Angola na kushiriki katika uzinduzi wa hospitali iliyopewa jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, zinaonesha kutambua mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Angola.
KUUNGANISHA USAFIRI NA BIASHARA
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji kwa kuunganisha Shoroba ya Lobito nchini Angola na Shoroba ya Kati inayounganisha maeneo mbalimbali na Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema uunganishaji huo utakwenda sambamba na juhudi za kukamilisha ukarabati wa Reli ya TAZARA kwa upande wa Tanzania na Zambia, pamoja na Reli ya Benguela nchini Angola, inayounganisha eneo la Lobito kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia.
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha biashara kati ya nchi hizo na maeneo mengine ya bara la Afrika.
Vilevile, amesema nchi hizo zimetia saini makubaliano ya huduma za usafiri wa anga yatakayowezesha kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Luanda, hatua inayotarajiwa kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa pamoja na kukuza utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.
Amesema kwa sasa wasafiri wanaotoka Tanzania kwenda Angola hulazimika kupitia nchi nyingine, hali inayoongeza muda na gharama za safari.
KUSHIRIKIANA KATIKA KUTAFUTA AMANI
Kwa upande wa masuala ya kikanda na kimataifa, Rais Samia amesema viongozi hao wamejadili hali ya usalama na utulivu katika eneo la Kusini mwa Afrika na Ukanda wa Maziwa Makuu, wakieleza wasiwasi kuhusu migogoro inayoendelea katika baadhi ya maeneo, hususan mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Amesema wamejadili namna ya kuunga mkono juhudi za kutafuta amani na kutatua migogoro inayoendelea katika ukanda huo.
Aidha, amesema amemweleza Rais Lourenço kuhusu jukumu lake la kuwa kinara wa masuala ya afya ya mama na mtoto katika Umoja wa Afrika (AU), akimwomba kushirikiana naye katika kuendeleza juhudi za kuboresha afya ya wanawake na watoto.
Hatua hizo zinaashiria dhamira ya Tanzania na Angola kuendeleza uhusiano wao wa kihistoria kwa kuimarisha diplomasia, biashara, uwekezaji, usafiri na ushirikiano katika masuala ya kikanda.
Naye Rais wa Angola, João Lourenço, amezitaka Tanzania na Angola kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ili kuongeza maendeleo ya mataifa hayo na kuboresha maisha ya wananchi, akisema nchi za Afrika hazipaswi kutanguliza ushirikiano na mataifa ya mbali huku zikiweka pembeni fursa zilizopo miongoni mwao.
Amesema pamoja na Tanzania na Angola kuwa na uhusiano wa kihistoria na kidugu, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ili nchi hizo ziweze kunufaika kwa pamoja kupitia rasilimali, uwezo na fursa zilizopo katika mataifa hayo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza ya kitaifa nchini Tanzania, Rais Lourenço amesema hakuna nchi inayoweza kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi kwa kutegemea uwezo wake pekee, hivyo ni muhimu kujenga ushirikiano imara wa kiuchumi na mataifa mengine, hususan ya Afrika.
Amesema wakati mwingine nchi za Afrika zimekuwa zikielekeza nguvu katika kuanzisha ushirikiano na mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia, huku zikitoa kipaumbele cha chini kwa nchi nyingine za Afrika ambazo pia zina fursa za kunufaishana.
“Angola na Tanzania zikizidisha uhusiano huu, nina hakika Angola itanufaika kwa kiasi kikubwa na Tanzania pia itanufaika,” amesema Rais Lourenço.
Ameeleza kuwa nchi hizo zimekuwa zikisaini mikataba ya ushirikiano na hati za makubaliano katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mikataba iliyosainiwa wakati wa ziara hiyo, hatua inayolenga kuweka msingi wa kisheria utakaorahisisha ushirikiano kati ya serikali hizo na wadau wengine.
KUJENGA USTAWI WA WANANCHI
Rais Lourenço amesema baada ya kipindi cha mapambano ya ukombozi, jukumu la sasa la viongozi wa Afrika ni kuelekeza nguvu katika maendeleo ya kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Afrika unapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa mataifa hayo yana rasilimali na fursa zinazoweza kutumika kwa manufaa ya pande zote.
Ameeleza kuwa kuimarisha ushirikiano huo kutahitaji kuendeleza mikataba iliyopo, kuweka mifumo inayorahisisha utekelezaji wa makubaliano na kuhakikisha kuwa uhusiano wa kidiplomasia unazaa matokeo halisi katika biashara, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.
Rais Lourenço amesema Tanzania na Angola zina nafasi ya kuongeza manufaa yatokanayo na uhusiano wao kwa kuimarisha ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Amesema hatua hiyo itasaidia nchi hizo kutumia fursa zilizopo ndani ya Afrika badala ya kutegemea zaidi washirika kutoka nje ya bara hilo.













