NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema kupitia mfumo wa NeST makundi maalumu ya wazawa wenye ulemavu,wanawake,wazee na vijana yanaweza kuomba hadi zabuni za Sh.Bilioni 50/- kutokana na sheria ya Ununuzi wa Umma kuweka upendeleo maalum.
Pia imetoa upendeleo wa hadi asilimia 10 kwa wazabuni wa ndani kwenye zabuni ambazo zinahusisha ushindani wa kimataifa.
Kadhalika imetoa upendeleo wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa za ndani ya nchi dhidi ya bidhaa za nje ya nchi.
Upendeleo huo si kwa maneno tu, bali kupitia Mfumo wa NeST ambao ni rahisi kufuatilia na kutekeleza, kwani wazabuni wa nje hawawezi kubofya kitufe cha kuomba zabuni zenye thamani ya chini ya Sh Bilioni 50 kwa kuwa zimewekwa kwa ajili ya wazabuni wazawa pekee.
Kadhalika upendeleo kwa Makundi Maalum Sheria ya Ununuzi wa Umma, imezielekeza taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya Kundi hilo maalumu.
Hii inatokana na Sheria mpya ya mwaka 2023 na Kanuni za mwaka 2024 ambayo PPRA imekabidhiwa dhamana ya kusimamia na kufuatilia uzingatiaji wa sheria katika ununuzi na ugavi wa umma nchini.
Aidha katika kutekeleza jukumu hilo kuu, PPRA imelenga kuhakikisha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha kwenye michakato ya ununuzi wa umma, Kuhakikisha uzingatiaji wa haki, ushindani, uwazi, uendelevu, uwajibikaji, matumizi mazuri ya fedha, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi;Kuwa na viwango bora na mahsusi vya mifumo ya ununuzi wa umma na ugavi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Dennis Simba wakati wa Kikao Kazi baina yake na Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo Alhamisi Oktoba 29,2026 jijini Dar es Salaam.
“Tumeshaanza na NeST kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoa upendeleo kwa kampuni za wazawa katika zabuni za bidhaa, kazi za ujenzi na huduma;Kuhakikisha wadau wote wa ununuzi (taasisi nunuzi na wazabuni) wanazingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, na Kanuni zake za Mwaka 2024, pamoja na miongozo inayotolewa na PPRA; na Kuwajengea uwezo wadau wa ununuzi wa umma, kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana na masuala ya ununuzi na ugavi (na sasa ni Wizara ya Fedha)” amefafanua Simba
Amesema takribani asilimia 70 ya bajeti yote ya Serikali inatumika kupitia ununuzi wa umma, maarufu kama tenda za Serikali. Kiasi hiki kinaelekezwa katika kuhakikisha kuwa wazabuni ambao ni wananchi wa ndani ya Tanzania, pamoja na wale wazabuni wa nje ya nchi wanatumia fursa hii kutekeleza miradi na kazi za Serikali. Hivyo, ni fursa ya kufanya biashara na Serikali wakati umepewa dhamana ya kutoa huduma kwa maslahi ya Taifa letu.
“Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan ilitumia fursa ya maendeleo ya teknolojia katika kuhakikisha usimamizi bora wa sekta hii ya ununuzi wa umma. Ili iwe na tija, ifanikishe kuwa na miradi inayoakisi thamani halisi ya fedha, kupunguza muda wa michakato ya ununuzi, kupunguza gharama za michakato na kuongeza uwazi na usawa. Hivyo, Mwaka 2023, Serikali ya Awamu ya Sita ilikamilisha ujenzi wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), na mfumo huu ukaanza kutumika rasmi Septemba 2023 kama njiaa pekee ya kutangaza na kuchakata Tenda za Serikali na Taasisi zake. ”
Amesema ,Mfumo huo uliojengwa na Wazawa umekuwa na matokeo makubwa na kuleta mapinduzi makubwa na muhimu kwenye sekta ya ununuzi wa umma nchini.
“Na hapa nasisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, michakato yote ya ununuzi wa umma inatakiwa kufanyika ndani ya Mfumo wa NeST. Hadi sasa tayari moduli kuu sita (6) ambazo ni moduli ya usajili wa watumiaji (e-Registration), moduli ya kuendesha michakato ya ununuzi (e-Tendering), moduli ya malipo ya mikataba (e-Payment), moduli ya usimamizi wa mikataba (e-Contract Management) na moduli ya katalogia (e-Catalogue); moduli ya ununuzi kupitia mnada wa kielektroniki wa kushusha bei (e-Reverse Auction), zimekamilika na zinaendelea kutumika,na kuboreshwa kutokana na maboresho ya maoni ya watumiaji na mahitaji mapya.
“Kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Mfumo wa NeST unasomana na mifumo zaidi ya Therathini (30), ikiwa ni pamoja na mifumo ya kibenki, mifumo ya malipo, mifuko ya hifadhi za jamii, bodi za usajili wa wataalamu, mifumo ya leseni na Mfumo wa upekuzi wa Mikataba ya Ununuzi na mingine mingi. ” amefafanua Simba
Mbali ya hayo Simba ameeleza kuwa hatua hiyo imesaidia kuondoa kabisa uwezekano wa kuwa na nyaraka za kughushi kwenye Mfumo wa NeST; lakini pia kurahisisha mchakato wa kuwasilisha nyaraka husika wakati wa ushiriki wa zabuni.
“Napenda kueleza zaidi kuhusu moduli ya usimamizi wa mikataba, ambayo ni moduli kubwa zaidi kwenye Mfumo wa NeST. Kupitia moduli hii ya usimamizi wa mikataba, Utayarishaji wa mkataba (contract preparation),upekuzi wa mikataba (contract vetting) mpaka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na kusaini mkataba husika vinafanyika ndani ya Mfumo wa NeST.
” Yaani, mkataba unasainiwa bila kuchapisha karatasi, ni kidijitali ndani ya Mfumo. Aidha, katika jitihada za kuimarisha ufanisi na usalama wa michakato ya ununuzi wa umma, Mamlaka imeendelea kuunganisha Mfumo wa NeST na mifumo ya kibenki ili kuwezesha uhakiki wa dhamana za zabuni au za benki (Bid Securities / Bank Securities) kufanyika moja kwa moja kupitia Mfumo wa NeST.”amejinasibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa PPRA
Akizungumza kuhusu PPRA kusomana na mifumo mingine Simba amesema hadi sasa, Mfumo wa NeST umeunganishwa na Benki ya NMB, huku benki za TCB na CRDB zikiwa katika hatua za mwisho za kuunganishwa.Vilevile Mamlaka imeanzisha Mfumo wa Bank Security Portal, ulioanza kutumika Oktoba 1, 2026, unaowezesha benki nyingine zote kutoa na kuthibitisha dhamana za zabuni kupitia NeST bila kuhitaji kuunganisha mifumo yao moja kwa moja.
Pia Simba amesema hatua hiyo imepanua wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo, ambapo hadi sasa zaidi ya benki 36 zimeunganishwa kupitia Bank Security Portal. Maboresho haya yamerahisisha uhakiki wa dhamana za zabuni, kupunguza muda wa uchakataji na kuimarisha uwazi, usalama na ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma.
“Pamoja na moduli hizi kubwa, zipo moduli ndogo ndani ya Mfumo wa NeST, ikiwemo moduli ya usimamizi wa malalamiko ya rufaa na moduli ya ukaguzi na ukidhi. Kwa upande wa moduli ya usimamizi wa Malalamiko na Rufaa za Zabuni za Umma ndani ya Mfumo wa NeST, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA), sasa wazabuni ambao wana malalamiko wanapata huduma kwa haraka kupitia Mfumo wa NeST.
” Malalamiko yao yanawasilishwa moja kwa moja na kufanyiwa kazi, kisha majibu yote yanawekwa pia kwenye Mfumo kwa uwazi na haki. Lakini pia moduli ya ukaguzi na ukidhi imejikita katika kuhakikisha kuwa Mfumo wa NeST uko salama.
“Na moduli hii tunaisimamia kwa ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).” ameongeza Simba
Akizungumzia mafanikio yatokanayo na matumizi ya Mfumo wa NeST tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo,Simba amesema wamepata mafanikio makubwa yanayoakisi maendeleo ya Taifa letu. Kwanza, ni kupanda kwa kiwango cha ukidhi wa sheria. Kutokana na matumizi ya Mfumo, taasisi zimelazimika kufuata utaratibu ili kukamilisha michakato ya ununuzi. Hivyo, kiwango cha ukidhi wa sheria kimeongezeka kutoka asilimia 65 (2023/24), asilimia 76 (2024/25), na kufika asilimia 79 (2025/26).
Amebainisha kuwa wamefanikiwa kuondokana na matumizi ya karatasi Matumizi ya Mfumo wa NeST yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Sh.Bilioni 27.64.Kuwaondolea wazabuni gharama na muda: Mfumo wa NeST umeondoa ulazima wa wazabuni kusafiri kupeleka nyaraka za zabuni kwa Taasisi nunuzi. Hatua hii pia imepunguza gharama na muda wa kushiriki michakato ya ununuzi wa umma.
“Hivi sasa, mzabuni anaomba zabuni popote alipo. Ufanisi na Athari za Kimazingira: Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonesha kuongezeka kwa ufanisi, uwazi, na kupungua kwa uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO₂e) kwa kiasi cha tani 64,768 kwa mwaka 2023/2024 hadi 2024/25.Utafiti wa Biashara ya Kaboni: Utafiti mkubwa unaendelea kufanyika ili kufanikisha usajili wa Mfumo wa NeST katika biashara ya kaboni, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuchangia zaidi ya Shilingi bilioni 20 kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.
“Ongezeko la Wigo wa Ushiriki wa Wazabuni, na utoaji wa zabuni kwa makundi maalum Matumizi ya Mfumo wa NeST yamewezesha kuwa na ushiriki mkubwa zaidi wa wazabuni, kwa kutoa zabuni kuanzia ngazi ya juu, ya kati hadi ngazi ya msingi (Serikali za Mitaa).
“Hivi sasa, kupitia Mfumo wa NeST, hata mafundi wa kawaida tu wanaweza kuomba na kupata kazi ya kushiriki ujenzi katika miradi ya Serikali. Pia, zabuni za hadi ngazi ya msingi, zinatolewa kwa haki na usawa kupitia Mfumo wa NeST. Hapa nazungumzia ununuzi katika ngazi za shule, vituo vya afya, ofisi za kata n.k. ” ameongeza
Katika hatua nyingine Simba amesema kuwa,Mfumo wa NeST umewezesha utekelezaji wa upendeleo wa zabuni na bidhaa za ndani ya nchi ambapo
hadi sasa, makundi maalum 33,659 yamesajiliwa kwenye Mfumo wa NeST. Ambapo makundi ya vijana ni 16, 133 wanawake 16,070, wazee 767 na watu wenye ulemavu 689.
Amesema makundi maalum yamepata zabuni zenye jumla ya thamani ya Sh.Bilioni 82.34, kupitia Mfumo wa NeST. Ambapo makundi ya vijana yamepata zabuni zenye thamani ya Sh.Bilioni 44.74, wanawake 33.15, wazee Bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Milioni 680.21.
Simba anesema kuwa,Lengo la PPRA, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni kuwa na takribani makundi 300,000 yaliyo tayari kuomba zabuni.
“Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kutoa ajira na kazi kwa Watanzania ambao hawana uwezo wa kuwa na kampuni, ambao wanaweza kujiunga kwenye vikundi na kutekeleza zabuni husika ya kazi na ajira 3,000,000″amefafanua Simba
Ameeeleza kuwaKutokana na nia ya kuwainua Watanzania kiuchumi, Kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh. Milioni 500.
Sambamba na hayo yote Simba ametumia fursa hiyo kutoa wito tena kwa Watanzania, kuchangamkia fursa hizi za ununuzi wa umma ili tuweze kujenga taifa letu na kujiinua kiuchumi. Tukishiriki kikamilifu kwenye ununuzi wa umma, tunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kuwa nchi ya Uchumi wa Kati kikamilifu








