NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, amesema ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi, itafungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, hususan katika biashara, uwekezaji, kilimo, miundombinu, afya, elimu na sayansi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi na mgeni wake leo Jumamosi Julai 18, 2026, Dk. Samia amesema ujio wa Rais El-Sisi, aliyeambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji, unatoa fursa ya kujadili kwa kina namna bora za kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliodumu kwa miaka mingi kati ya Tanzania na Misri.
Amesema moja ya vielelezo vikubwa vya ushirikiano Kati ya nchi hizo mbili ni utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye thamani ya Sh trilioni 7.4, uliojengwa na kampuni mbili kutoka Misri kwa kutumia fedha za ndani za Tanzania.
“Mradi huu ni uthibitisho kwamba nchi za Afrika zikiamua zinaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa uwezo wao wenyewe na bila kutegemea ushiriki wa nje ya bara la Afrika,” amesema.
Kuhusu biashara na uwekezaji, Dk. Samia amesema pande zote zimekubaliana kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Misri bado ni kidogo licha ya kuwepo kwa fursa kubwa za kukiongeza.
Amesema Misri ni ya nane kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania, ikiwa na miradi 61 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5 iliyozalisha ajira zaidi ya 4,000 katika sekta za nishati, viwanda, ujenzi, kilimo, utalii na huduma nyingine.
Aidha, amesema wafanyabiashara 35 kutoka Misri wameambatana na Rais El-Sisi na wanakutana na wenzao wa Tanzania kupitia jukwaa la biashara, hatua inayotarajiwa kuongeza biashara na uwekezaji kwa kutumia fursa za Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Katika sekta ya kilimo, Rais Samia amesema Afrika hutumia kati ya dola za Marekani milioni 70 hadi milioni 100 kila mwaka kuagiza chakula kutoka nje, hususan ngano, mahindi, mchele, mafuta ya kula, sukari, nyama na maziwa.
Amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa chakula ndani ya bara.
Amesema Tanzania ina hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na ni nchi ya pili barani Afrika kwa idadi ya mifugo, huku Misri ikiwa imepiga hatua kubwa katika teknolojia za umwagiliaji kutokana na matumizi ya Mto Nile.
Kwa msingi huo, amesema Serikali ya Misri imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania kuendeleza Ranchi ya Ruvu, ambayo kwa sasa haijatumika kikamilifu, kwa lengo la kuifanya kuwa kitovu cha uzalishaji wa kisasa wa mifugo na uwekezaji wa pamoja.
Rais Samia pia amewahamasisha wawekezaji kutoka Misri kushirikiana na taasisi za Serikali zenye maeneo makubwa ya uzalishaji, ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Magereza, Shirika la Taifa la Ranchi (NARCO), pamoja na miradi ya kilimo inayotekelezwa Zanzibar.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira kwa Watanzania na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao na mifugo kwa soko la Afrika na masoko mengine ya kimataifa.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, hali inayoweka mazingira mazuri kwa uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa chakula kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amefafanua kuwa Tanzania na Misri zimefikia makubaliano ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji wa baharini kwa kuunganisha bandari za mataifa hayo mawili, hatua inayolenga kuongeza biashara, kuvutia uwekezaji na kupanua masoko ndani ya Afrika na ukanda wa Ghuba.
Rais Samia alisema ushirikiano huo utahusisha pia maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa eneo maalumu la kuhifadhi bidhaa na makontena ya Misri katika Bandari ya Bagamoyo, ambalo litaunganishwa na reli hadi Kwala ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.
Amesema pande zote mbili zimekubaliana kuendeleza mazungumzo ya kuunganisha Bandari za Dar es Salaam, Bagamoyo, Safaga pamoja na bandari nyingine za Misri, jambo litakalorahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza gharama za biashara na kuongeza ushindani wa mataifa hayo katika soko la kimataifa.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mpango huo utafungua njia kwa bidhaa za Tanzania kuingia kwa urahisi zaidi katika masoko ya nchi za Ghuba, huku bidhaa kutoka Misri zikipata fursa ya kufikia nchi za Afrika Mashariki na Kusini kupitia bandari za Tanzania.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, Rais Samia amesema Rais El-Sisi ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara wakubwa 35 wanaoshiriki Jukwaa la Biashara Tanzania na Misri, hatua inayotarajiwa kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha, amesema Shirika la Ndege la EgyptAir tayari linaendesha safari tatu kwa wiki kati ya Misri na Tanzania, huku akiihimiza Air Tanzania kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Misri ili kurahisisha usafiri wa abiria, kukuza utalii na kuongeza fursa za biashara.
Rais Samia amesisitiza kuwa ushirikiano huo unaipa Tanzania nafasi ya kuendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, huku ukiimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na Misri




