NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
UWEKEZAJI katika mafunzo na maendeleo ya wanawake ni hatua muhimu ya kuwaandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi, huku kukisisitizwa umuhimu wa kuweka mifumo inayowapa fursa za kutumia uwezo wao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Riziki Pembe Juma wakati akifungua Jukwaa la Uongozi wa Wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi likiwa na kaulimbiu inayohimiza kukuza na kudumisha uongozi wa wanawake kwa muda mrefu barani Afrika.
Amesema mafunzo kwa viongozi wanawake ni muhimu katika kuwajengea ujuzi, kujiamini na uwezo wa kufanya maamuzi, kutatua changamoto na kusimamia mipango ya maendeleo.
Kupitia mafunzo hayo, wanawake wanaweza kuimarisha utendaji wao na kujiandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Mafunzo kwa viongozi wanawake licha ya kuwajengea ujuzi, kujiamini na uwezo wa kufanya maamuzi, pia huwasaidia kutambua fursa zilizopo, kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma na kujiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika nafasi za uongozi,” amesema
Dk. Juma amesema kuimarisha nafasi za wanawake katika uongozi kutasaidia kuongeza uwakilishi wao katika vyombo vya maamuzi na kuhakikisha mitazamo na mahitaji ya makundi mbalimbali ya jamii yanazingatiwa katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Aidha Dk. Juma amesisitiza kuwa kufikia usawa wa kijinsia kunahitaji mifumo inayotekelezeka, sera zinazowezesha wanawake kupata fursa sawa na juhudi za pamoja za serikali na wadau mbalimbali katika kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kupiga hatua katika uongozi.
Vilevile, amesema mipango ya maendeleo inapaswa kuzingatia ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha makundi hayo yanapata nafasi ya kuchangia katika maamuzi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050 imetajwa kuwa miongoni mwa nyenzo zinazolenga kuweka msingi wa maendeleo jumuishi, ikiwemo kuimarisha fursa za wanawake kushiriki katika uongozi na maendeleo ya taifa.
Hivyo, ameeleza kuwa uwekezaji katika uwezo wa wanawake na kuweka mazingira yanayowawezesha kushiriki katika nafasi za maamuzi ni muhimu katika kujenga taasisi zinazozingatia mahitaji ya jamii na kuharakisha maendeleo endelevu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu katika sekta tofauti, ikiwemo wanawake walio katika nafasi za uongozi.
Amesema kati ya washiriki 400 wa programu moja ya mafunzo, 390 walihitimu, huku mshiriki mmoja akishindwa kuhitimu kutokana na sababu ambazo hazikuelezwa, akieleza kuwa taasisi hiyo inatarajia kuona washiriki wa programu zinazoendelea wakihitimu katika mahafali yajayo.
Singo amefafanua kuwa taasisi hiyo inaendesha programu nne kuu za mafunzo ya uongozi ambazo ni Stashahada ya Uzamili ya Uongozi (Postgraduate Diploma in Leadership), inayodumu kwa mwaka mmoja, programu ya Wanawake katika Uongozi (Women in Leadership), Cheti cha Uongozi (Certificate in Leadership) na programu ya Kuandaa Viongozi (Making Leaders Program).
Ameeleza kuwa programu hizo zimekuwa sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuimarisha uwezo wa viongozi, kuwapa maarifa ya kukabiliana na changamoto za uongozi na kukuza ujuzi wa kitaaluma.
Aidha, amewashukuru washirika na wafadhili wanaoiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake, akiwataja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza mafunzo na programu zinazolenga kujenga viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taasisi wanazoziongoza.
Naye Naibu Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women) nchini Tanzania, Jolly Acen amesema uongozi wa wanawake ni haki ya msingi na nguzo muhimu katika kujenga taasisi jumuishi zinazowajibika na zinazozingatia mahitaji ya wananchi wote.
Amesema kuwa pamoja na kupanua fursa kwa wanawake, ni muhimu pia kuondoa vikwazo vinavyowakabili katika maendeleo yao ya kitaaluma, ikiwemo ubaguzi na unyanyasaji mahali pa kazi.
Kwa mujibu wa Acen amesema changamoto hizo zinahitaji hatua za kitaasisi zinazoambatana na sera zilizo wazi, rasilimali za kutosha na mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kuendeleza uwezo wao na kufikia nafasi za juu za uongozi.
Aidha, Acen amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwawezesha wanawake katika hatua mbalimbali za taaluma zao kupitia mafunzo ya kitaaluma, ushauri elekezi, udhamini wa maendeleo ya kazi na mitandao ya kitaaluma inayowaunga mkono.
Katika kutekeleza azma hiyo, shirika hilo limesema limekuwa likishirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Taasisi ya Uongozi kupitia programu ya uongozi wa wanawake inayolenga kuimarisha ujuzi wa uongozi wa kimabadiliko na uwezo wa wanawake kushawishi maamuzi.
Pia, limeunga mkono mafunzo ya uongozi kwa wanawake wanaoshiriki katika uongozi wa kisiasa kuanzia ngazi ya Bunge hadi mamlaka za serikali za mitaa, kwa lengo la kuongeza uwezo, kujiamini na ufanisi wao katika kutekeleza majukumu ya uongozi.




