
NA MUNIR SHEMWETA,NEW YORK,MAREKANI
SERIKALI ya Tanzania imetaja vipaumbele vitatu vitakavyoiongoza kuharakisha utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji (New Urban Agenda) hadi mwaka 2036, vikilenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora na nafuu, kuboresha huduma za msingi pamoja na kuimarisha ushiriki wa serikali za mitaa na wananchi katika maendeleo ya miji.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, wakati akiwasilisha taarifa ya Tanzania katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat) kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji kwa kipindi cha miaka 10, mwishoni mwa wiki katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

SEHEMU ya washiriki wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat) kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji kwa kipindi cha miaka 10, uliomalizika mwishoni mwa wiki katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Akizungumza katika jopo la majadiliano lenye kaulimbiu “Delivering for People: Scaling Adequate Housing, Land, Basic Services and Inclusion,” Mhandisi Sanga alisema Tanzania imeendelea kupanua upatikanaji wa makazi bora na ya gharama nafuu kupitia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kurasimisha makazi yasiyopangwa na kuongeza maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya makazi.
‘’Serikali ya Tanzania imefanya maboresho ya sera na mifumo ya kisheria ili kuwezesha uwekezaji katika sekta ya makazi, huku wananchi wakiruhusiwa kujenga nyumba zao baada ya kupata kibali cha mipango miji na ujenzi’’. amesema Mhandisi Sanga
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na taasisi zake ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za aina mbalimbali kwa ajili ya kuuza na kupangisha, huku akisisitiza kuwa suluhisho la changamoto za makazi halitegemei ujenzi pekee bali pia linahitaji haki salama za umiliki wa ardhi, mifumo bora ya usimamizi wa ardhi, upatikanaji wa fedha za makazi na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeeleza mafanikio yake katika kuanzisha mifumo bunifu ya kufadhili maendeleo ya miji, ikisema hatua hiyo inaweka msingi wa kuhakikisha ukuaji wa kasi wa miji unakwenda sambamba na upatikanaji wa huduma bora, miundombinu ya kisasa na maendeleo endelevu kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Sospeter Mtwale wakati akiwasilisha mada kuhusu “Unlocking Delivery: Financing Sustainable Urbanization at Scale in Tanzania”,
Amesema,Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini, hususan katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Arusha, kutokana na fursa za ajira, biashara, elimu na huduma za afya, jambo linaloongeza mahitaji ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maendeleo ya mijini.
Kwa mujibu wa Mtwale, changamoto kubwa inayozikabili nchi zinazoendelea si ukuaji wa miji pekee, bali ni namna ya kupata vyanzo vya uhakika vya fedha vitakavyowezesha utekelezaji wa miradi ya nyumba, miundombinu na huduma za msingi kwa njia jumuishi, himilivu na endelevu, sambamba na kufanikisha Ajenda Mpya ya Miji (New Urban Agenda).
Amesema katika hatua za kukabiliana na changamoto hiyo, Tanzania imeanza kutumia mbinu mbalimbali za kibunifu ikiwemo Hatifungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji ya Tanga (Tanga Water Infrastructure Green Bond), iliyowezesha kupatikana kwa dola za Marekani milioni 20.8 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji, huku ikionesha kuwa mamlaka za serikali za mitaa zinaweza kutumia masoko ya mitaji ya ndani kugharamia miradi ya maendeleo.

