NA MWANDISHI WETU,MAKAMBAKO,NJOMBE

IMEELEZWA kuwa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na mbolea imewawezesha wakulima nchini kujiandaa kununua na kutumia mbolea kulingana na mahitaji halisi ya udongo na zao husika na hivyo kuongeza tija mashambani pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima kwa mkulima.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 17,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),Joel Laurent wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya mamlaka ya kukagua na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa uliofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.
Akizungumza katika ghala la kampuni ya OCP Tanzania Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TFRA amewasisitiza wakulima kutojihusisha na ununuzi wa mbolea nje ya mfumo wa ruzuku na kueleza mbolea zote zinapatikana kupitia mfumo huo na zinawafikia wakulima kwa bei elekezi.
Naye Ofisa Udhibiti Ubora wa TFRA, Heneriko Renatus, amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi zake ikiwemo TFRA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kupitia kampeni ya “Mali shambani” inayolenga kuwajengea uwezo wakulima katika kuboresha shughuli zao za kilimo.
Ameeleza kuwa, kupitia kampeni hiyo wakulima wanahimizwa kutumia lishe linganifu kwa viwango sahihi katika hatua za kupandia, kukuzia na kuzalishia, ili kuhakikisha mimea inapata virutubisho kwa wakati unaofaa.
Kwa upande wake, Meneja wa OCP Makambako, Charles Modest, amesema kwa sasa ghala la kampuni hiyo lina tani 3,000 za mbolea na limepokea tani 2,000 nyingine za mbolea za kupandia aina ya TSP na NPSZN, zitakazosambazwa kwa Mawakala na wakulima wa Mkoa wa Njombe na wilaya zake.





