NA MWANDISHI WETU, KALAMBO,RUKWA

KATIKA kuadhimisha kilele cha Siku ya Mbolea Duniani, 2025 Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Kampuni za Mbolea Nchini, imeendelea na kampeni ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima kwa kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Kampeni hiyo ilianza kutekelezwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya na Rukwa, kwa kuwafikia wakulima mashambani kuwapa elimu sahihi ya mbolea, kuzingatia kanuni nne za matumizi ya mbolea na kuwakumbusha umuhimu wa kutumia mbolea ili kuzalisha kwa tija pamoja kupima afya ya udongo.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Samson Poneja, ameeleza kuwa kilimo kimeimarika Nchini, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 560,551 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 1,323,799 mwaka 2024/25.

Ameongeza kuwa matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 363,598 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 972,074 mwaka 2024/25.

“Tunawahimiza wakulima kuendelea kujisajili katika mpango wa ruzuku ili waweze kununua mbolea na mbegu kwa bei nafuu na kupima afya ya udongo. Kumbuka, ukiitaka mali utaipata shambani,” ameeleza Poneja

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Nicholaus Eliadu, ameipongeza Wizara ya Kilimo na Serikali kwa ujumla kwa kampeni hiyo na mpango wa ruzuku ya mbolea ambapo amesema imeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima wa eneo hilo.

“Tunaishukuru sana Wizara ya Kilimo kwa kampeni hii ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwani imekuja kwa wakati tunapoelekea msimu wa kilimo. Kupitia kampeni hii, wakulima wa Kalambo watahamasika kutumia mbolea kwa usahihi zaidi ili kuongeza tija na uzalishaji,” alisema Eliadu.

Naye mkulima wa maharagwe katika Halmashauri ya Kalambo, Benard Agustino, ameeleza kufurahishwa na elimu hiyo na namna ruzuku ya mbolea ilivyoboresha mavuno yake.
“Kabla ya ruzuku, nilikuwa napata gunia kati ya sita hadi tisa pekee za mahindi. Lakini sasa baada ya kutumia mbolea kwa kufuata elimu tuliyopewa, napata gunia 15 hadi 20 kwa msimu,” amesema Agustino.

Agustino aliwahimiza wakulima wenzake kuendelea kujisajili kwenye mpango wa ruzuku ya mbolea na kutumia mbolea ipasavyo, akisema hatua hiyo inaleta tija kubwa katika kilimo na ustawi wa kaya zao.

Maadhimisho ya siku ya Mbolea Duniani kote hufanyika Oktoba 13 kila mwaka ili kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea na hivyo kuchochea uzalishaji na kuongeza tija.

