NA MWANDISHI WETU,TABORA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), mwishoni mwa juma lililopita imeendesha karakana ya mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea na uchaguzi wa mbegu bora za mazao kwa wakulima wa vijiji vya halmashauri za Manyoni, Itigi, Ikungi, Singida MC, Mkalama na Iramba.
Steven Gossi ,Ofisa Udhibiti Ubora Mwandamizi kutoka TFRA amewasihi wakulima kuzingatia kanuni za matumizi sahihi ya mbolea ikiwa ni pamoja kubaini aina ya mbolea inayohitajiwa na udongo kabla ya matumizi.
Baada ya mafunzo, wakulima wameeleza kuwa, awali walikuwa wakitumia mbolea bila kuzingatia kanuni za matumizi sahihi ya pembejeo hiyo ikiwa ni pamoja na kutokutofautisha baina ya mbolea ya kupandia na ile ya kukuzia jambo lililopelekea kuambulia mavuno kidogo sana.
Kufuatia Kampeni inayoendelea ya Mali shambani, jamii ya wakulima na wazalishaji wa mazao wataondokana na changamoto za kiuchumi na kijamii kwani sasa watazalisha kwa tija kwa ajili ya chakula na biashara.



