NA MWANDISHI WETU,BUNDA,MARA
WAKULIMA wa zao la mpunga katika kijiji cha Mariwanda, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani hapa wamepatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kupitia Kampeni ya ‘Mali Shambani’, inayolenga kuongeza uzalishaji,ubora wa mazao na kuinua kipato cha wakulima kuelekea msimu wa kilimo 2025/2026.
Elimu hiyo inatolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi zake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha Sekta ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanatumia pembejeo kwa ufanisi unaozingatia mahitaji halisi ya udongo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa Kilimo wa Chama cha Ushirika mkoani Mara,(WAMACU), Daniel Chacha, amesema matumizi sahihi ya mbolea ni nyenzo muhimu katika kuongeza mavuno ya mpunga na kulinda rutuba ya ardhi.
Amesisitiza umuhimu wa wakulima kuchagua mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na kuzingatia viwango vinavyopendekezwa na wataalamu.
Kwa upande wake, Ofisa Udhibiti Ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Godwin Vedastus, amewahimiza wakulima kutumia mbolea zenye ubora na zilizosajiliwa rasmi, akibainisha kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu na kufanya ukaguzi ili kuhakikisha mbolea inayowafikia wakulima ni salama na inakidhi viwango vinavyotakiwa.
Mkulima wa mpunga kutoka kijijini hapo, Philipo Maige, amesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea katika kuongeza mavuno na kuboresha ubora wa mazao.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa maelekezo ya wataalamu unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika uzalishaji msimu ujao.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanaonesha kuwa kilimo chenye tija kinahitaji elimu sahihi, matumizi bora ya pembejeo na ushirikiano kati ya wakulima, wataalamu wa kilimo na taasisi za udhibiti, ili kufikia maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo.












