NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATOTO 300 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji na wataalamu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia.
Upasuaji huo umefanyika kwa awamu tisa tangu mwaka 2019 ambapo awamu hii watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kati ya watoto 50 waliofanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu ya siku 10 iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo leo jijini Dar es Salaam Balozi wa Saudi Arabaia nchini Tanzania Yahya Bin Ahmed Okeish alisema huduma za upasuaji wa moyo zinazofanyika kwa watoto zimedhamiria kuwarejeshea uhai watoto ambao wanasumbuliwa na magonjwa hayo.
Okeish aliwapongeza wataalamu ambao wamekuwa wakichukua muda wao kutoka nchini Saudi Arabia kuja Tanzania kwaajili ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto na kuwataka kuendelea na moyo huo wakujitoa.
“Niwapongeze wataalamu wa Afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na wale wa kituo cha misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia kwa kujitolea kurudisha tabasamu kwa watoto hawa”, alisema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Abdallah Kilima alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaishukuru Serikali ya Saudi Arabia kupitia Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman kwa kuwaruhusu wataalamu wake kutoa huduma kwa watoto wa Tanzania.
Balozi Kilima alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia kuhakikisha huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto zinaendelea kutolewa hasa katika familia ambazo haziwezi kumudu gharama za matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo Dk. Tatizo Waane aliseme Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman kimeweza kuchangia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.5 tangu waanze kushirikiana na JKCI ambapo awamu hii wamechangia shilingi milioni 700.
Dk. Waane alisema kambi ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu kutoka kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman imekuwa ikitoa huduma kwa watoto wengi kwa kipindi cha muda mfupi hivyo kupunguza idadi ya watoto wanaosubiri upasuaji wa moyo.
Kwa niaba ya wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo Ester Benazedi alitoa shukrani kwa wataalamu waliotoa huduma ya upasuaji kwa watoto 30 akiwemo mtoto wake aliyekuwa na tundu kwenye moyo pamoja na mishipa yake ya damu kuwa myembamba.
Benazedi alisema mtoto wake aliteseka kwa muda mrefu ila baada ya kufanyiwa upasuaji anaendelea vizuri na sasa anaweza kucheza na wenzake.
“Nawashukuru sana wataalamu hawa wa JKCI na wenzao kutoka Saudi Arabia kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wangu ambaye sasa anaendelea vizuri Mungu awabariki”, alisema Benazedi