NA MWANDISHI WETU, UKEREWE
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ukerewe imemhukumu Diwani wa Kata ya Illangala Petro Majula kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya Ufujaji, Ubadhirifu pamoja na Matumizi Mabaya ya Mamlaka.
Makosa hayo ni kinyume na vifungu vya 28 (1) pamoja na 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022], vikisomeka pamoja na Aya ya 21, Jedwali la kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ilivyofanyiwa
Marejeo mwaka 2022.
Hukumu dhidi ya Misana imetolewa Agosti 5, 2024 kutokana na Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 02/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Lucas Nyahenga.
Shauri hili liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza Moses Malewo.
Awali ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kushindwa kuwasilisha kiasi cha Sh. 5,198,546.80 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, fedha ambazo alizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbali mbali vya mapato vya Halmashauri hiyo akiwa wakala wa kukusanya mapato.
Duwani Majula alifanya hivyo huku akijua ni kinyume na Memoranda ya Fedha za Halmashauri za Mwaka 2009 lakini pia ni Kinyume na Sheria ya Fedha za Halmashauri Sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, ambapo Sheria hizi zote zinamtaka kila anayekusanya mapato ya Halmashauri kuyawasilisha kwenye akaunti za Halmashauri kila siku anapokusanya ama kesho yake endapo kuna changamoto.