NA ANDREA NGOBOLE,ARUSHA
BAADHI ya vifungu vya kanuni za maudhui mitandaoni, katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) zimepingwa katika mahakamana ya Afrika yaMashariki, kwa kudaiwa vimekiuka misingi ya haki za binaadamu na mkataba wa jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Mashirika manne ya utetezi wa haki za binaadamu nchini, Kituo cha sheria na haki za binaadamu (LHRC) baraza la habari Tanzania (MCT), Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) na taasisi ya Center for strategic litigation ndio yamefungua kesi hiyo dhidi ya mwanasheria mkuu wa Serikali.
Kesi hiyo imesikilizwa Alhamisi Novemba 13 katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki, mbele ya Majaji watano, Jaji Johanes Masara, jaji Richard Wejuri, jaji Richard Muhumuza, Jaji Dk. Gacuko Leonard na Kayembe Kasanda.
Mawakili upande wafungua maombi katika shauri hilo namba 30/2020 Wakili Jeremiah Mtobesya na wakili Peter Majanjala, waliiomba Mahakama hiyo, kutamka vifungu hivyo, ni batili kwakuwa vinakiuka misingi ya haki za binaadamu na mkataba wa jumuiya hiyo.
Wakili Mtobesya akiwasilisha hoja zao katika shauri hilo, alisema sheria yoyote ambayo inatungwa inapaswa kuzingatia misingi ya haki za binaadamu, ikiwepo uhuru wa kutoa taarifa na kupokea taarifa lakini baadhi ya kanuni za sheria hiyo licha ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2022 na 2025 lakini bado vina mapungufu.
Alisema vifungu vya kanuni za maudhui mtandaoni namba 3,4,5,6 na vingine kadhaa katika sheria hiyo ya EPOCA vinakiuka misingi ya haki za binaadamu, lakini pia havipo wazi katika makosa ya kusambaza maudhui ambayo yanayotajwa yakitendeka na hivyo kutoa nafasi kutumika vibaya.
“Kuna suala la kutoa adhabu ya faini ya sh.Milioni 5 au kifungo cha miezi 12 kwa ambaye atatiwa hatiani kwa makosa ya kimaudhui adhabu hii ni kubwa mno na inanyima fursa watu kutoa maoni yao kwa uhuru katika mitandao”alisema
Kwa upande wake, Wakili Majanjala alisema kuna suala la utoaji wa leseni za maudhui mtandaoni pia ni changamoto kwani sio kila ambaye anatoa maudhui mtandao anatumia maudhui hayo kibiashara, lakini pia kuna mapungufu katika utoaji wa leseni hiyo.
Alisema kanuni hizo, pia zinakiuka mkataba wa jumuiya ya Afrika ya Mashariki, katika vifungu namba 6d, 7, 8(c) ambavyo pamoja na mambo mengine vinaelezea uongozi bora ikiwa ni pamoja na kuzingatia sera za demokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi, haki ya kijamii, fursa sawa, usawa wa kijinsia pamoja na kutambua, kukuza na kulinda haki za binadamu.
Alisema hivyo, wanaomba mahakama hiyo, kutamka wazi kuwa vifungu hivyo, vinakiuka Katiba ya jumuiya hiyo na Misingi ya haki za binadamu hasa uhuru wa kujieleza, kupokea taarifa na kutoa taarifa .
Hata hivyo Mawakili wa Serikali Waandamizi wakiongozwa na Wakili Stanley Kalokola na Daniel Nyakiha wakijibu hoja za waleta maombi, walieleza mahakama hiyo kuwa, vifungu vingi ambavyo vinalalamikiwa tayari vimefanyiwa marekebisho na serikali.
Wakili Kalokola alisema kanuni hizo za Maudhui hazikiuki misingi ya haki za binaadamu ikiwepo haki ya kutoa taarifa na kupokea taarifa.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Johanes Masara, alisema siku ya kutoa hukumu ya shauri hiyo itatolewa.
Shauri hilo imesikilizwa katika mahakama hiyo, ikiwa ni shauri la nne ndani ya wiki moja , ikihusiana na masuala ya haki za binaadamu katika mahakama hiyo pia imesikiliza shauri namba 25 na 27/2020 ambayo yameunganishwa yaliyofunguliwa na chama cha mawakili wa Afrika, (PALU) THRDC, LHRC kuhusu kupinga sheria ya mtu akitaka kufungua kesi za kikatiba na shauri na 28/2020 la Abdul Omar Nondo dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali.
Mahakama hiyo, imeeleza itapanga siku ya kutoa hukumu hizo baada ya kuwaita waliofungua kesi na ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali.


