NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala mkoani hapa imewatia hatiani Viongozi wa Kamati ya Urasimishaji Makazi eneo la Kipunguni ‘A’ katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Ahmed Msika na wenzake watatu kwa kosa la ubadhirifu na ufujaji wa fedha kinyume na kifungu Cha 28(2) Cha PCCA [Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022].
Washtakiwa wengine ni Humphrey Mwakalinga, Mohammed Magwila na Kisura Byakuzana.
Hukumu hiyo ya kesi ya jinai namba CC.386/2024 ilitolewa Julai 5 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Gloria Nkwera, katika shauri lililoendeshwa na Mawakili Waandamizi wa Serikali Veronica Chimwanda na Fatuma Waziri.
Ilielezwa mahakamani hapo Msika na viongozi wenzake walifuja Sh.Mil.10/- zilizokuwa zimekusanywa na wananchi kwa ajili ya urasimishaji wa makazi yao.
Hata hivyo baada ya hukumu kutolewa Washtakiwa walifanya makubaliano (Plea bargaining) na walilipa fedha hizo serikalini na kuamriwa kutokufanya makosa yanayofanana na waliyoshtakiwa nayo kwa kipindi cha miaka mitatu.