Aeleza jitihada za Serikali kupunguza changamoto ya umeme
Aipongeza Mbeya kwa utekelezaji miradi ya maendeleo
Asisitiza siasa zisiwagawe wananchi
NA TERESIA MHAGAMA, MBEYA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko, leo Februari 19,2023
amewasili mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi mkoani humo.
Ziara hiyo pia itahusisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani humo.
Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Dk. Biteko
amepokelewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Juma Homera.
Katika kikao chake na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Biteko ameeleza
jitihada zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo
Elimu, Siasa na Nishati.
Katika Sekta ya Nishati, Dk. Biteko ameeleza kuwa, upungufu wa umeme
nchini ni kati ya megawati 300 hadi 190 lakini kwa sasa kuna
matumaini makubwa kwani mradi wa Julius Nyerere ( JNHPP) unatarajiwa
kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa mwezi huu na matumaini
mengine ni kutoka Mradi wa umeme wa Rusumo ambao utaingiza katika
gridi megawati 27.
Amesema kuwa, kiasi hicho cha umeme kitakapoingia kwenye gridi ya
Taifa kitaondoa hali ya sasa ya mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko
uzalishaji na pia kuiwezesha Serikali kuendelea kufanya maboresho
kwenye miundombinu ya umeme.
Amesema kuwa, kwa Mkoa wa Mbeya ambao mahitaji yake ni kati ya
megawati 70 na 74 ambapo kwa sasa wanapata umeme wa megawati 51 na
kueleza kuwa, jitihada zinazoendelea sasa zitapelekea Mkoa huo pia
kupata umeme kulingana na mahitaji.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amepongeza Mkoa wa Mbeya kwa
kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi ya
maendeleo pamoja na usimamizi mzuri wa sekta Elimu ambao watoto
wanaostahili kwenda shule wameripoti kwa zaidi ya asilimia 70.
Vilevile, Dk. Biteko amesisitiza viongozi kufuata agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwa,
tofauti ya itikadi ya vyama vya siasa isifanye wananchi kuwa maadui
bali watu wabishane kwa hoja huku kipaumbele kikiwa ni maendeleo ya
nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amemueleza Dk.
Doto Biteko kuwa, shughuli za kiuchumi katika Mkoa huo zinaendelea
vizuri na katika mwaka 2023/2024 walifanikiwa kukusanya mapato ya
Sh. Bilioni 49 ikiwa ni zaidi ya asilimia 105.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi ya umeme inaendelea vizuri
ikiwemo ya upelekaji umeme vijijini, vitongojini na migodini.
Katika elimu amesema kuwa, Mkoa huo umekuwa na ufaulu mzuri huku
watoto wanaopaswa kwenda shule, wakiripoti kwa zaidi ya asilimia 70.