NA HAPPINESS SHAYO, DODOMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amewaelekeza Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kuhakikisha wanashughulikia madai ya wananchi ya muda mrefu ya kifuta jasho na kifuta machozi.
Ameyasema hayo leo Februari 15,2024 katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma.
“Hatungependa kuona wananchi wana madai ya muda mrefu. Muangalie taarifa zenu za madai na muende uwandani mkajiridhishe vizuri ili kujua kama mna taarifa sahihi au la.” Kairuki amesisitiza.
Aidha, amewataka watendaji hao kupitia upya mfumo wa utoaji taarifa pale mwananchi anapopata madhara kuanzia mtu anapopata tukio anaripoti vipi, kwa nani na kujiridhisha kama mfumo huo ni rafiki kwa mwananchi wa kawaida ambaye hana elimu.
“Ninataka kuona haki inatendeka kwa wote wenye elimu na wasio na elimu wakiwa wamepoteza mazao au wamejeruhiwa wajue wapi kwa kuripoti” Waziri Kairuki amesema.
Waziri Kairuki amewahimiza watendaji hao kutengeneza utaratibu wa utoaji elimu kwa umma na pia kusambaza miongozo mbalimbali katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Vijiji ili kuwepo na uelewa wa pamoja pindi mwananchi anapopata madhara yatokanayo na wanyama wakali na waharibifu.
Pia, amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Awali, akizungumza na Wabunge wa Mikoa ya Arusha na Manyara, Mhe. Kairuki amewaahidi kuzifanyia kazi changamoto zao zinazohusiana na migogoro baina ya wananchi na hifadhi, kifuta jasho na kifuta machozi, ujirani mwema na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu operesheni mbalimbali zinazofanywa na wahifadhi katika maeneo yao.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula baadhi ya Wabunge wa Mikoa ya Arusha na Manyara, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).