NA HAPPINESS SHAYO, DODOMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali itaendelea kutatua migogoro mbalimbali ya Sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo iliyo katika maeneo ya hifadhi kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Ameyasema hayo Februari 14,2024 katika kikao kati yake na Wabunge wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma, kwa lengo la kusikiliza changamoto zilizopo kwenye majimbo yao.
Amefafanua kuwa si vema kwa Serikali kuendelea kuwa na migogoro ya hifadhi kwa kipindi kirefu na si afya kwa Taifa, hivyo Serikali itafanya jitihada za kuitatua.
Kufuatia hatua hiyo, amewaelekeza Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kufanya tathmini ya kina kuhusu migogoro iliyopo katika maeneo yao na kuangalia namna bora ya kuitatua.
“Ninawaelekeza Watendaji wote kila mmoja akaijue migogoro yake, aangalie nini kimefanyika na kipi cha kufanya kumaliza migogoro hiyo” Kairuki amesisitiza.
Aidha, amewaahidi wabunge hao kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii itaongeza jitihada katika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na kushirikiana nao katika utatuzi wa migogoro inayojitokeza katika maeneo yao.
Kuhusu uadilifu wa Watendaji na Askari Uhifadhi, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo zaidi na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa uadilifu na kuwapatia vitendea kazi ili waweze kujua wanatakiwa kufanya nini kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Pia, amesema Wizara itaendelea kutangaza namba za Watendaji ili kurahisisha utendaji kazi inapotokea changamoto waweze kuchukua hatua kwa wakati na iwe rahisi kwa wananchi kutoa taarifa.
Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti Wabunge wa Mikoa hiyo wamempongeza Waziri Kairuki kwa uamuzi wake wa kusikiliza changamoto zao.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (Mb), baadhi ya Wabunge wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).