*Waweka mikakati ya kutatua changamoto za Nishati EAC
* Bajeti za Nishati EAC zatakiwa kuongezeka
*Tanzania yapitishwa kuwa Mwenyeji wa Kongamano la Petroli la Afrika Mashariki
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
MKUTANO wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ulioanza Februari 12, 2024 katika Makao
Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha umehitimishwa jana .
Katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Shaibu
Kaduara ambaye ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar
ulipendekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na
kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya
usambazaji na usafirishaji.
Aidha, Mkutano huo ulitoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha
upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa
maendeleo ya Jumuiya na watu wake.
Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara alieleza kuwa, Jumuiya itaweza
kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na
biashara endapo pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikanaji wa
nishati ya uhakika na salama.
“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha maendeleo
ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya, hivyo umuhimu wa upatikanaji
wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na
sio hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa
na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na
kimataifa”. alieleza Waziri Kaduara
Vilevile, Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki katika hafla
ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP)
utakaofanyika Februari 25, 2024.
Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa ngazi ya Makatibu
Wakuu ambao ulipitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo
ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya. Pia ulipokea na kujadili taarifa za
maendeleo ya sekta ya nishati katika maeneo ya umeme, mafuta, gesi na
nishati jadidifu.
Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ambaye ni Katibu Mkuu wa
Wizara inayohusika na masuala ya Afrika Mashariki katika Jamhuri ya
Kenya, Abdi Dubati alieleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada
za Wakuu wa Nchi wanachana wa Jumuiya za kuhahikisha sekta ya nishati
inaimarika ili kuchagiza maendeleo ya Jumuiya kutokana na mchango wake
mkubwa katika kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na uzalisha wa
bidhaa viwandani.
Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo
Mhandisi Felchesmi Mramba ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati
alieleza kuwa, kikao hicho kinatoa fursa ya kuunganisha nguvu na
kuweka mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
nishati ikiwemo umeme.
Katika Mkutano wa ngazi ya Watalaam kulijadiliwa taarifa mbalimbali za
maendeleo ya sekta ya nishati katika Jumuiya. Vilevile kuweka mikakati
ya pamoja ya kutatua chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili
kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na endelevu katika
Jumuiya.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa ngazi ya wataalam
Mwenyekiti wa Mkutano huo, Petro Lyatuu, Mkurugenzi wa Sera na Mipango
katika Wizara ya Nishati – Tanzania alieleza kuwa, licha ya mafanikio
yaliyofikiwa katika sekta hiyo bado mchango na weledi wa wataalam hao
unahitajika ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kufikia
malengo yanayotarajiwa na Jumuiya.
Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambapo uliipitisha Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli
Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika Machi 7 hadi 9 Machi 2025.
Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta
binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya
sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya,
na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan
fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.