NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB)
imezindua kampeni maalum ya kuwawezesha Watanzania kufikia ndoto zao kupitia suluhisho sahihi za kifedha, lengo ni kukuza biashara, kuongeza kipato na kuchochea uchumi wa taifa.
Kupitia kampeni hiyo, TCB inalenga kuwafikia wajasiriamali, wakulima na familia kwa karibu zaidi, kuwapatia huduma za kifedha zitakazowawezesha kukuza shughuli zao na kuboresha maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi TCB, Jema Msuya amesema benki hiyo imejipanga kuwa mshirika wa kimkakati kwa wateja wake kwa kuwapatia huduma zitakazowawezesha kufanikisha malengo yao.
Amesema kampeni hiyo ni ya miezi mitatu na itafanyika Tanzania nzima kwa lengo la kuendelea kuwaelimisha watanzania jinsi ya kutimiza ndoto, kutoa msaada wa mawazo pamoja na kutoka elimu ya fedha na mikopo.
Naye Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano, Alex Dwashi amesema kampeni hiyo itaanzia Dar es Salaam na kisha kwenda mikoa yote nchini huku akisisitiza umuhimu wa mikopo yenye riba nafuu.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi Al-Amin Lwamo amesema kampeni hiyo itahisisha kuwafikia wajasiriamali moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia mikopo itakayoongeza mitaji yao na ufanisi wa uzalishaji hatua itakayosaidia kukuza pato la taifa, ajira na uchumi endelevu.



