NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
HISTORIA ya Tanzania katika harakati za kupigania uhuru, kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na mchango wake katika ukombozi wa Afrika ni miongoni mwa vivutio vitakavyopewa nafasi ya kipekee katika Maonesho ya Kiswahili yatakayofanyika jijini Paris, Ufaransa, sambamba na Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa.
Maonesho hayo yatakayofanyika katika viunga vya Makao Makuu ya UNESCO kuanzia Julai 4 hadi 7, 2026, yanatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kuendeleza matumizi ya Kiswahili na kuonesha mchango wake katika amani, mshikamano na diplomasia ya uchumi duniani.
Kwa mujibu wa mwongozo wa kongamano hilo, sehemu maalum ya maonesho itajikita katika kuonesha historia ya uhuru wa Tanzania, hatua za kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na nafasi ya Tanzania katika kuunga mkono harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika yaliyokuwa chini ya ukoloni.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ni miongoni mwa taasisi za Serikali chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, zitakazotuma uwakilishi wa kushiriki kwa mara ya kwanza katika kongamano hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Juni 11,2026 kuhusu Kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amesema lengo la kutuma uwakilishi wa Taasisi ni kujifunza uzoefu wa kimataifa, kuimarisha ushirikiano na wadau wa lugha na vyombo vya habari kutoka mataifa mbalimbali pamoja na kuendeleza mchango wa Tanzania katika kukuza Kiswahili.
Washiriki watapata fursa ya kujifunza mchango wa Tanzania katika kujenga mshikamano wa Afrika na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia diplomasia, huku vielelezo mbalimbali vikionesha nafasi ya taifa hilo kama kitovu cha harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Katika kuongeza mvuto wa maonesho hayo, nukuu za viongozi mashuhuri wa Tanzania, akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, zitaoneshwa kupitia skrini kubwa kwa lengo la kuhamasisha maadili ya uongozi, amani, umoja na maendeleo.
Aidha, maonesho hayo yataangazia mchango wa lugha ya Kiswahili katika diplomasia ya Afrika na nafasi yake katika kuimarisha utangamano wa watu wa mataifa mbalimbali, sambamba na juhudi zinazoendelea za kukitangaza Kiswahili kama lugha ya kimataifa inayobeba historia, utamaduni na utambulisho wa Waafrika.
Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa linaandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO chini ya kaulimbiu ya “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani,” likiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Julai 7.

