NA MWANDISHI MAALUMU, DODOMA
·
·
·
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Doto Biteko ameiagiza
Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha
zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa
ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania na wazingatie kutoa
kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.
Amesema hayo leo Februari 7, 2024 Jijini Dodoma katika hafla ya
utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi (NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki
wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum katika masuala ya
ununuzi wa umma.
“ Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya
Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka
makundi maalum. Na haya ni maelekezo ya Rais wa Tanzania, DkSamia
Suluhu Hassan ya kuhakikisha watanzania wote wanashiriki kwenye
shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali
na Binafsi wawezesheni watanzania kushika uchumi wa nchi na muone
fahari katika hili.”Amesema Dkt. Biteko
Kupitia hafla hiyo Dk.Biteko ameitaka PPRA kuzidi kuboresha huduma
zake kwa Watanzania ikiwa ni Pamoja na kuharakisha mchakato wa rufaa
zinazowasilishwa kwenye mamlaka hiyo hususani zile zinazohusisha
waombaji wa zabuni kutoka makundi maalum ili kuchochea kasi ya ukuaji
wa Uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye Uchumi wa Taifa. Amezitaka
mamlaka hizo kujikita zaidi katika uwezeshaji wa wananchi kwa kutoa
elimu badala ya kubaki kuwa wadhibiti pekee.
Ameziagiza NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa
huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala
litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma na hatmaye kukuza
Uchumi.
Amesema makubaliano hayo yatatumika kama jukwaa la kuwahamasisha watu
wa kundi hilo kushiriki na kuimarisha Uchumi wa mtu mmoja mmoja,
kuimarisha wigo wa walipakodi na hivyo kukuza Uchumi wa nchi.
Ameipongeza PPRA kwa kuweka kanuni ya ushirikishaji makundi maalum
kwenye manunuzi ambayo imeelekeza kuwa asilimia 30 ya zabuni zote
zitolewe kwa washiriki kutoka makundi maalum ambao ni wanawake,vijana,
Wazee na wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na
Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, amesema kusainiwa kwa hati ya
makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum
kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.
Amesema kuwa, makubalinao hayo yataongeza ushiriki wa makundi maalum
kwenyenunuzi ya umma na hii itaongeza uwezo wa watanzania katika
uzalishaji malighafi na bidhaa pamoja na utoaji wa huduma ndani ya
nchi.
Amesema kuwa, katika suala hilo la watanzania kushiriki katika kukuza
uchumi wa Taifa, Ofisi anayoisimamia itaendelea kuisimamia NEEC ili
iendeelee kuratibu utekelezaji wa sheria na hasa zile zinazohusu
ushiriki wa watanzania kwenye miradi mbalimbali na kujenga uchumi wa
nchi,
Waziri wa Fedha, DK.Mwigulu Nchemba amesema kuwa, kusainiwa kwa
hati hiyo kutaondoa mapungufu yaliyokuwa yakijitokeza kwenye masuala
ya ununuzi wa umma hasa kwa watu wenye makundi maalum hivyo baada ya
kusainiwa kwa hati hiyo utekelezaji wake utaanza mara moja.
Amesema siku zote Serikali inalenga katika kuwawezesha wananchi
kiuchumi hali itakayoongeza walipakodi na hasa kwa watu
wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi na wenye uwezo badala ya
wananchi wa hali ya chini.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Baadhi ya Naibu mawaziri, Makatibu
Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri wa Mkuu (Sera, Bunge
na Uratibu), Dk.Jim Yonaz, baadhi ya Wabunge na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda.