NA MWANDISHI WETU,RUANGWA,LINDI
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesema inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kukuza uchumi wa nchi, na itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata huduma na fursa mbalimbali zinazohitajika katika shughuli zao.
Akifunga Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Mkoa wa Lindi kwa mwaka 2026, yaliyofanyika katika Wilaya ya Ruangwa leo Septemba 19, 2026, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, amesema Wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya madini.
“Ninawaomba wachimbaji kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na taasisi zake ili kuboresha shughuli zao na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema Dk. Kiruswa.
Aidha, Dk. Kiruswa amewahimiza wachimbaji wa madini kuzingatia Sheria ya Madini, sheria za mazingira, afya na usalama mahali pa kazi, pamoja na taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali katika shughuli za uchimbaji.
Ametoa wito kwa taasisi zinazohusika, ikiwemo OSHA, NEMC, Tume ya Madini na Halmashauri, kuendelea kutoa elimu na kusimamia shughuli za uchimbaji ili kuhakikisha zinafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia misingi ya uendelevu
Pia, Dk. Kiruswa amesema maonesho hayo yamekuwa fursa kwa wananchi kujifunza na kutambua fursa zilizopo katika sekta ya madini, huku akiwahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuutazama Mkoa wa Lindi kama eneo lenye fursa za uwekezaji katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini.
“Mkoa wa Lindi unaendelea kujenga nafasi muhimu katika sekta ya madini nchini kutokana na uwepo wa madini mbalimbali. Kwa hiyo, ninawahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuutazama Mkoa wa Lindi kama eneo lenye fursa za uwekezaji,” amesema Dk. Kiruswa.
Sambamba na hayo, Dk. Kiruswa amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha Mkoa wa Lindi unakuwa na kiwanda cha kuchakata madini ya nikeli, pamoja na kuimarisha masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji kupata masoko ya uhakika na kupunguza changamoto za uuzaji wa madini yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, amesema mkoa huo unatambua mchango mkubwa wa sekta ya madini katika maendeleo ya Mkoa wa Lindi, na umejipanga kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji na wawekezaji.
Naye Muwakilishi wa Wabunge wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, ameiomba Serikali kuongezan viwanda vya uchenjuaji wa madini ya nikeli na shaba ili kuongeza thamani na tija ya madini hayo katika Mkoa wa Lindi.







