NA BENNY MWAIPAJA,DODOMA
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amefungua vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya kuchachua na kutengemaza uchumi kupitia sekta za uzalishaji.
Alitumia fursa hiyo kulishukuru Shirika hilo kwa kutoa fedha zinazotumika kutekeleza miradi inayosaidia kuchochea maendeleo ya wananchi, kukuza uchumi jumuishi na kuiwezesha nchi kuhimili misukosuko ya kiuchumi inayoikabili dunia.
Dk. Nchemba alisema kuwa kiasi cha takriban Sh. Tril.1.3 kilichotolewa na Shirika hilo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya uviko 19 na kiasi kingine cha shilingi trilioni 2.8 kitakachotolewa na IMF kwa awamu saba kwa miaka mitatu kuanzia mwaka wa Fedha 2022/2023 hadi mwaka wa fedha 2024/2025, kimeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi na huduma za kijamii katika sekta za afya, maji, kilimo, ujenzi wa miundombinu, uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara.
“Tunaishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya IMF kwa kuidhinisha tathimini ya awamu ya pili ya ECF mwezi Desemba mwaka 2023 na kutoa kiasi cha dola za Marekani 150.5 milioni na kufanya nchi ipokee jumla ya dola za Marekani 455.3 milioni za mpango wa ECF kwa awamu mbili hadi sasa.” alisema Dk.Nchemba
Alitumia pia nafasi hiyo kuiomba IMF, kuisaidia Serikali kupata fedha kupitia dirisha lake la Resilient and Sustainable Trust (RST), kwa ajili ya kusaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Mimi na timu yangu tupo tayari kwa mazungumzo na kuweka malengo yanayopaswa kutimizwa ndani ya muda ambao tutakuwa tumeshauriana ili kuweza kutekeleza program ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi”, alisema Dk. Nchemba.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu hiyo ya IMF Harris Charambos Tsangarides, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza kwa umahili mpango wa ECF na kutimiza vigezo vilivyoweka katika mpango huo kwa wakati na kusaidia nchi kupata kiasi cha dola za Marekani 150.5 mwezi Desemba mwaka 2023.
Akijibu maombi ya Waziri wa Fedha kuhusu upatikaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Tsangarides, alisema kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kupata fedha hizo na kushauri kukamilisha maandalizi ya awali kwa wakati ikiwemo tathimini ya sera za nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuingia katika majadiliano na IMF mwezi Aprili 2024.