NA TERESIA MHAGAMA, TANGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko leo Januari 26,2024
amefanya ukaguzi wa mitambo ya umeme inayokarabatiwa katika kituo cha
umeme cha New Pangani (MW 68) ambacho kilisimama kuzalisha umeme kwa
zaidi ya wiki mbili kutokana na hitilafu na kuwaagiza Wataalamu
waTANESCO kufanya kazi hiyo kwa kasi na umakini ili kukamilisha
matengenezo hayo ambayo yapo ukingoni.
Katika ziara yake kwenye kituo hicho kilichopo wilayani Korogwe
mkoani Tanga, Dk. Biteko aliambatana na viongozi mbalimbali akiwepo
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba.
“ Nawapongeza kwa hatua mliyofikia sasa kwenye matengenezo, lakini ni
muhimu sana kuongeza kasi na umakini katika kumalizia kazi kwani
Watanzania wanatutegemea sisi ili kupata umeme wa uhakika.” amesema
Dk.Biteko
Dk. Biteko ameeleza kuwa, matengenezo ya kituo hicho yapo ukingoni na
inategemewa kuwa wiki ijayo kitaanza tena kuzalisha umeme na hivyo
kuimarisha hali ya upatikanaji umeme hasa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro
na Arusha.
Aidha ameongeza kuwa, jitihada nyingine zinazofanyika ili kuimarisha
hali ya umeme kwenye mikoa hiyo ni kupitia laini ya msongo wa kV 400
itakayotoka Chalinze- Segera hadi Tanga Mjini na laini ya kV 400
kutoka Singida – Manyara- Lemuguru ambayo itaunganishwa na laini ya
kutoka Chalinze kwenda Segera hadi Tanga Mjini.
Vilevile, Dk.Biteko amewataka watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa,
wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya umeme, jambo
litakalowawezesha kutambua mapema endapo kuna hitilafu za umeme na
kuzifanyia kazi mapema.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amewasha umeme katika Kijiji
cha Ngomeni kata ya Ngomeni wilayani Muheza, Mkoa wa Tanga, na kufanya
vijiji vilivyowashiwa umeme wilayani Muheza kufikia 127 kati ya Vijiji
135 sawa na asilimia 95 na katika Vitongoji, Wilaya ya Muheza ina
vitongoji 522 na hadi kufikia jana vitongoji 411 vilikuwa
vimesambaziwa umeme huku kazi hiyo ikiendelea.
Mara baada ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho, Dk. Biteko amesifu
umoja uliopo kati ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali
katika Mkoa huo, na kueleza kuwa, siri ya mafanikio ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ni viongozi kama hao wanaochapa kazi kwa umoja.
Amesema kuwa, viongozi wanapogawanyika wanachelewesha maendeleo na
kuwaumiza wananchi kwani wananchi wanachohitaji ni huduma bora kama za
umeme na maji, hivyo amewaasa viongozi kupendana na kushirikiana,
kwani wanapimwa kwa matokeo ya maendeleo.
Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa
nyakati tofauti wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuwajali wananchi na kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya Maendeleo ambapo mpaka sasa Mkoa wa Tanga umepokea
shilingi Trilioni 2.6 kwa ajili ya miradi ya miradi ya Maendeleo.
Fedha iliyotengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini wilayani
Muheza ni Sh. Bilioni 18.96 ambayo ni kwa ajili ya kusambaza
umeme kwenye nyumba, migodi midogo, vituo vya afya, maeneo ya kilimo
na pampu na za maji huku Mkandarasi akiwa ni kampuni ya Derm Group.