NA MWANDISHI MAALUMU, MBEYA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu Furaha Issa [32] mkazi wa Iwambi, Goodluck Mwakajisi [25] na Azimio Gerlad [31] Mwalimu Shule ya msingi Mwanselela, mkazi ZZK – Mbalizi kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, uporaji, uvunjaji wa nyumba na wizi.
Watuhumiwa walikamatwa Januari 25, 2024 katika misako iliyofanyika maeneo mbalimbali ya Mji Mdogo wa Mbalizi na kukutwa na mali mbalimbali za wizi, televisheni 2, redio Subwoofer 3, redio ndogo 4 na spika zake, deki 4, laptop 2, chaja za laptop 8, simu za mkononi 16, remote 11 za TV na Redio, bidhaa mbalimbali za dukani, mashine 1 ya kupimia shinikizo la damu, mashine 1 ya kupimia damu na vyombo vya kupikia.
Aidha, watuhumiwa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia nyumba na maduka, visu 4, mapanga 3. Baadhi ya mali zimetambuliwa na wahanga, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kufika kituo cha Polisi Mbalizi kwa ajili ya kutambua mali zao.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtuhumiwa Nazareth Mangwale [36] mkazi wa Mwaselela akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi gram 15 kwenye pochi yake.
Mtuhumiwa alikamatwa Januari 25, 2024 maeneo ya Utengule katika Mji Mdogo wa Mbalizi katika Misako iliyofanywa na Jeshi la Polisi katika maeneo hayo. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa bhangi, taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea.


