NA TERESIA MHAGAMA
MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas ameeleza kuwa, ziara
aliyofanya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko
mkoani Mtwara Novemba 14 na 15, 2023 imeleta matokea chanya
kwani maagizo yote aliyoyatoa yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo mitambo
ya umeme ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa muda mrefu sasa imeanza
kuzalisha umeme.
Amesema hayo wilayani Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati wa
hafla ya uwekaji saini Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia
itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma kilichopo
mkoani Mtwara na uwekaji saini hati ya Makubaliano kwa ajili ya
kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza Gesi Asilia
kwa teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa
Kimiminika (Mini-LNG).
Amesema kuwa, Dk.Biteko akiwa mkoani Mtwara alifanya ziara
katika kituo cha umeme mkoani humo na kukuta mitambo miwili ya umeme
haifanyi kazi kwa muda mrefu ambapo alitoa agizo kwa TANESCO
kuhakikisha mitambo hiyo inatengemaa na kuanza kuzalisha umeme ili
kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme.
Ameeleza kuwa, kutokana na agizo hilo la Dk.Biteko, mitambo hiyo
imefanyiwa ukarabati na sasa inafanya kazi na kuongeza megawati 6.5
kwenye mzunguko.
Ameongeza kuwa, kazi ya ujenzi wa eneo ambalo litawekwa mtambo
mwingine wa megawati 20 mkoani humo unaendelea kwa kasi kubwa hali
itakayozidi kuimarisha hali ya umeme na kuchochea uwekezaji.
Vilevile amesema kuwa, kazi ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha Afya
katika Kijiji cha Msimbati inaendelea na hii inatokana na ziara ya
Dk Biteko katika visima vya kuzalisha Gesi Asilia na mitambo ya
kuchakata gesi iliyopo Mnazi Bay, Kata ya Msimbati ambapo aliagiza
wananchi katika eneo hilo wapate huduma bora ikiwemo ya Afya,
Barabara na pia kupata gawio la ushuru wa huduma linaloenda kwenye
Halmashauri.
Ameongeza kuwa, kile anachokisisitiza Dk Biteko ni kuwa, miradi
inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi,
ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo
vya Afya, Barabara na Maji.
Katika hatua nyingine, Kanali Makame amemshukuru Rais, Dk Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati mkoani
Mtwara ikiwemo ya Afya, Miundombinu, Nishati na kwamba mradi huo wa
Gesi Asilia wa Kitalu cha Ruvuma unaotekelezwa mkoani Mtwara
wataulinda na kuutunza kwa ajili ya Wananchi mkoani Mtwara na Taifa
kwa ujumla.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko ameeleza
kufurahishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara
yake na hii inajumuisha maagizo aliyoyatoa wakati alipofanya ziara
yake katika Kisiwa cha Songosongo ambapo aliagiza masuala mbalimbali
ikiwemo ya wananchi kupatiwa usafiri wa uhakika utakaowawezesha kuvuka
maji kwenda wilayani Kilwa na pia kusambaziwa na kupatiwa umeme wa
uhakika.
Dk. Biteko amesema hali ya umeme katika Mkoa wa Lindi na Mtwara
itazidi kuimarika baada ya kuingia pia kwenye gridi ya Taifa ya umeme
kutokana na laini ya kV 220 inayojengwa kutoka Songea hadi
Mtwara-Lindi na hii inaenda na sambamba na ujenzi wa laini nyingine za
umeme katika maeneo tofauti ya nchi pamoja na ujenzi wa vituo vya
kupoza umeme.