NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amesema kuwa upo uwezekano wa kurudia baadhi ya vipengele vya Mradi wa LNG ili kuviboresha zaidi.
Aidha , Majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji wa Mradi wa LNG yapo katika hatua nzuri na wataalamu wanaendelea kupitia vipengele vya mkataba huo ili kuhakikisha kila upande unaridhika.
“Tunaendelea kupitia na kuboresha baadhi ya vipengele vya mkataba huu ili pindi utakapokuwa tayari uwe nyenzo ya kuhakikisha matarajio na manufaa ya mradi huu yanafikiwa,” alifafanua Dk. Biteko.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Septemba 13, 2023 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk Michael Battle katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.
Mbali ya hayo Dk Biteko alisema, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati ikiwemo ya uzalishaji umeme pamoja na Mradi wa kubadili Gesi Asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG).
Akizungumzia kuhusu suala hilo Dk. Biteko ameahidi kufuatilia kuhusu wawekezaji hao kutokana na uhitaji mkubwa wa Nishati ya Umeme hapa nchini kwa sasa.
Naye Balozi Battle alimtaarifu Dk. Biteko kuwa zipo kampuni mbili za Kimarekani Astra Energy na Upepo Energy zenye lengo la kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la uzalishaji umeme na tayari zimekwishawasilisha rasmi nia yao ya kuwekeza hapa nchini.
Vivyo hivyo Balozi Battle ameeleza kuwa ana imani Dk.Biteko atafanya vizuri katika kusimamia Sekta ya Nishati ikizingatiwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika Sekta ya Uziduaji ikiwa ni pamoja na uzoefu wa aina ya mikataba aliyokutana nayo kipindi akiwa Waziri wa Madini.
Pamoja na mambo mengine , Dk Battle amemtembelea Dk. Biteko kwa lengo la kumpongeza kwa uteuzi na majukumu yake mapya ikiwa ni pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili.