NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATOTO 439 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia tangu Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) kuanzishwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Kisenge wakati wa ziara ya Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania alipotembelea kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na madaktari hao kwa kushirikiana na wenzao wa JKCI leo Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam.
Dk.Kisenge alisema kambi inayofanyika hivi sasa jumla ya watoto 30 watapatiwa matibabu hadi hapo kesho ambapo kambi hiyo itakapomalizika na kuokoa gharama kama watoto hao wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Wenzetu kutoka nchini Saudi Arabia kupitia Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu wamekuwa wakishirikiana nasi tangu Taasisi hii ilipoanzishwa, mwaka wao wa kwanza kufika JKCI waliwafanyia upasuaji wa moyo watoto 100, hivyo hadi kufikia leo wanaweka idadi ya watoto 439”, alisema Dk.Kisenge
Dk.Kisenge alisema undugu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Saud Arabia umepelekea uhusiano wa kusaidia mahali ambapo uhitaji wa msaada unahitajika ususani kwa watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.
“Watu wengi hupoteza maisha kama hawajapata huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo, wenzetu wamekuwa wakiwasaidia watoto wetu na kuwaacha wakiwa na furaha baada ya kupatiwa matibabu”, alisema Dk.Kisenge
Aidha Dk. Kisenge alisema kuwa kupitia kambi hiyo madaktari wa JKCI wameweza kupata ujuzi zaidi hivyo kuiwezesha JKCI kuendelea kuwa na upekee Afrika Mashariki na kati huku wakiwasaidia watanzania na wale walio pembezoni mwa Tanzania kupata huduma za matibabu ya moyo kwa urahisi.
Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Yahya Okeish alisema ofisi ya ubalozi haina budi kuwashukuru madaktari kutoka Saudi Arabia kwa kutekeleza malengo ya kujitoa kuwasaidia watoto na kuwaleta faraja.
Balozi Okeish alisema Ufalme wa mfalme Salman unatekeleza miradi zaidi ya 5694 ya kutoa misaada ya kibinadamu katika maeneo zaidi ya 167 ikiwemo JKCI kuhakikisha watoto wenye magonjwa ya moyo na familia zao zinapata furaha.
“Madaktari hawa wameweza kutoka nchini kwao na kufika hapa Tanzania wakifuata maneno ya muumba wetu kuwa mtu akiokoa maisha ya mtu mmoja atakuwa ameokoa maisha ya watu wanne wanaomzunguka yule mmoja anayehitaji kuokolewa maisha yake”, alisema Balozi
Balozi alisema Kituo cha Mfamle Salman kinatoa huduma za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo bila ya kujali rangi, jinsi, au dini ndio maana kimeendelea kuwa msaada kwa watanzania tangu kuanzishwa kwa JKCI hadi sasa.
Naye mzazi ambaye mtoto wake amepatiwa matibabu katika kambi hiyo Janeth Njimba aliwashukuru madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kwapamoja kumfanyia upasuaji wa moyo mwanaye aliyekuwa na shida ya moyo.
“Naushukuru uongozi wa Rais Dkt. Samia, uongozi wa JKCI na uongozi wa mfalme Salman kutuletea jopo la wataalamu ambao wameshiriki vizuri katika kuwapatia tiba watoto wetu”, alisema Njimba
Aliomba ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia kuendelea kwani watoto wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo Tanzania bado ni wengi na wengi wao hawawezi kumudu gharama za matibabu hivyo wakiendelea kufanya upasuaji kwa msaada kutawasaidia watoto wengi.