NA MWANDISHI WETU, DODOMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini(REA) inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania bara vitafikiwa na huduma ya umeme.
Ameeleza hayo bungeni, jijini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Namikunda,
Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke.
Akijibu swali hilo, Kapinga alisema kuwa katika Jimbo la Masasi,
Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo
havikuwa na umeme ambapo hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2023, vijiji 11
vimeshawashwa umeme na vijiji 6 vitakamilika kabla ya mkataba wa
Mkandarasi kuisha tarehe 31 Desemba, 2023.
Aliongeza kuwa, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na
Chakama vimekwishawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia Desemba 31,
2023 Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa
umeme.
Alisema kuwa, kwa sasa, zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya
Temeke (Mkarango) bado linaendelea na nguzo tayari zimekwisha
simamishwa katika kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya
linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023