NA MWANDISHI WETU, DODOMA
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa ya mjini hapa, imefanikiwa kupandikiza uume kwa wanaume wawili waliopungukiwa nguvu za kiume.
Wataalamu wa hospital hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo nchini (TAUS) pamoja na Daktari Bingwa kutoka Ufaransa wamefanikisha upasuaji huo kwa wanaume hao ambao walikuwa na matatizo ya nguvu za kiume kwenye viungo vyao hivyo nyeti vilivyokuwa vinashindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.
Akiongea baada ya kukamilisha upasuaji Dkt. Remigius Rugakingira ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na Wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume.